Msiba tena! Sheikh Matata, hatunae

Aliwanyosha kwa hoja walioitilia shaka Qur’an

 

Na Bakari Mwakangwale

SHEIKH  Othman Matata , amerejea kwa Mola wake, huku akiwakumbusha Waislamu muhadhara wa mwaka 1987, katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.

Sheikh Matata, amefariki Alhamisi, usiku wa kuamkia Ijumaa ya wiki iliyopita (Mei 8,2020) na kuzikwa siku hiyo hiyo ya Ijumaa katika Makaburi ya Kisutu, Jijini Dar es Salaam.

Sheikh Matata, ameelezewa kuwa alikuwa mahari katika mahubiri katika Mihadhara akishirikiana na Marehem Sheikh Ngariba na Kawemba, hususana katika muhadhara wa Kwanza uliofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam mwaka 1987, na mada Kuu ilikuwa Dini moja, Mungu ni Mmoja.

Sheikh Matata, atakukmbukwa kwa umahadhiri wake katika mada za Mlingano wa Dini mbali mbali, kupitioa Mihadhara akiwa mtaalamu wa Fasihi ya Kingereza na fasaha katika uchambuzi wa Sayansi ya Quran ndani na nje ya Tanzania.

Marehemu Matata, amewahi kuwa katika jopo la Wahadhiri wakongwe nchini toka kipindi cha Marehem Sheikh Ngariba na Kawemba chini ya Marehem Sheikh Qassim Juma, katika Mihadhara iliyokuwa ikivuta hisia za Wakristo na Waislamu katika ya Viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam na baadae nchi nzima.

Mwenyekiti Kamati ya Mawasiliano Hizb ut Tahrir Tanzania Sheikh Mussa Kileo, amesema pamoja baada ya kufanya kazi kubwa ndani ya nchi Shekh Matata na timu yake waliweza kusafiri mbali mbali kwa kazi hiyo ambayo imeleta matunda kwa Uislamu.

Alisema, kupitia Mihadhara yao watu wengi waliweza kuujua Uislamu na Kusilimu na kuingia katika nuru ya Uislamu baada kubaini ukweli wa Uislamu kuwa ndio dini pekee ya kweli kwa Mwenyezi Mungu baada ya kupata dalili na hoja kutoka kwa Sheikh Matata na wenzake.

Amesema, Sheikh Matata, alikuwa ni miongoni mwa Wahadhiri wenye Elimu kubwa hivyo kifo chake ni pigo na pengo jengine katika uwanja wa elimu ya Kiislamu na Da’awah kwani alikuwa hodari, fasaha na mwenye uwezo wa kujenga hoja, hasa kwa wale wenye kujaribu kutilia mashaka Qur’an Tukufu.

“Hizb ut Tahrir Tanzania, inatoa mkono wa Ta'azia kwa Umoja wa Wahadhiri Tanzania,Waislamu wa Tanzania khaswa, familia, Masheikh, Maustadh, na Walimu kwa msiba wa kuondokea na nguzo kubwa ya Da’ awa na ulinganiaji katika Uislamu.” Amesema Sheikh Mussa Kileo.

Kwa upande wake, Sheikh Kondo Bungo, amemu elezea Sheikh Matata, kuwa alikua ni Muislamu mwenye grama ya kutisha katika lugha ya kiengereza ambapo alianza na uwanahabari akitangaza katika Radio Tanzania katika Idhaa ya Kiingereza.

“Baada ya hapo alizama katika uwanja wa Da’awah, katika ulinganiaji katika Mihadhara na huko alikua bingwa wa kuvunja hoja za aya mutashabihat hasa kwa Wakristo na Wanasayansi waliotaka kupindisha usahihi wake.”

“Na ilikuwa likitokea jambo gumu katika hoja watu humtumia kupata chochoro katika ulingo wa elimu ya hoja, amekufa akiwa ndie Mwenyekiti wetu wa Taasisi ya Almalid, Dar es Salaam. Allah (sw) ampe safari nyepesi Shekh Othman Matata, Aamin.” Amefafanua Sheikh Bungo.