Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Urusi imetangaza kuwa, nchi hiyo haitafumbia jicho vitisho vya makombora ya Marekani.
-
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Urusi kwa mnasaba wa hatua ya Marekani ya kujiondoa kwenye Mkataba wa Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati (INF) imesema kuwa, kuweka makombora ya nyuklia ya masafa mafupi na ya masafa ya kati ya Marekani katika maeneo mbalimbali duniani kunahatarisha sana amani ya kikanda na kimataifa.
Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Urusi imesema kuwa, hatua hiyo ya Marekani itaanzisha awamu mpya na hatari ya mashindano ya silaha.
Taarifa hiyo imesema kuwa, Urusi haiwezi kufumbia jicho vitisho zaidi vya makombora dhidi ya ardhi yake. Imesema njia pekee ya kimantiki ni kupatikana mwafaka kupitia njia za kisiasa na kidiplomasia.
Imesisitiza kuwa Urusi iko tayari kurejesha hali ya kuaminiana na kuimarisha amani ya kimataifa na ina matumaini kwamba, Marekani pia itachukua hatua za kimantiki na za kuwajibika katika uwanja huu.
Hivi karibuni, Marekani ilitangaza kujitoa kwenye mkataba wa pande mbili iliosaini na Urusi, wa kupiga marufuku silaha za nyuklia za masafa ya kati (INF).
Kufuatia hatua hiyo ya Marekani, Urusi nayo ilijibu mapigo na kuamua kujitoa kwenye mkataba huo.
Mnamo mwezi Juni 1987, Marekani na Urusi ya zamani zilisaini mkataba wa kupiga marufuku silaha za nyuklia za masafa ya kati INF, ambao ulianza kutekelezwa rasmi Juni 1988.
Makubaliano ya INF yalipiga marufuku Washington na Moscow kuweka makombora yao ya balestiki na cruise barani Ulaya.Parstoday.