Na Bakari Mwakangwale

WAKATI inaelekea kutimia miaka 50 toka kifo chake, inaonyesha Marehemu Abdulwahid Sykes, ni shujaa wa harakati za Uhuru wa Tanganyika aliyesa haulika katiki historia ya Taifa lake

Hali hiyo inajidhihirisha katika maelezo ya mwanae, Aisha Abdulwahid Sykes ‘Daisy’ akimuelezea baba yake wakati huu akielekea kutimiza miaka 50 tangu kufariki wake, akikumbuka harakati zake katika kutafuta Uhuru wa Tanganyika.

Marehemu Sykes, aliyezaliwa Januari 31, 1924 na kufariki dunia Oktoba 12, 1968, alikuwa mtu maarufu, kinara na mzalendo wa nchi yake katika harakati za kupigania Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara).

Aisha anasema, licha ya kwamba sasa ni nusu karne tokea kufariki kwake, bado baba yake amebaki kama kielelezo na rejea muhimu, kwani alikuwa akifahamika kama mtu wa watu kwa jinsi alivyokuwa mwepesi wa kukirimu wageni.

“Hali hii ilijitokeza zaidi Dar es Salaam, mji aliozaliwa kukulia na kufahamika kwa wengi, Tanganyika na nje ya mipaka yake watu kutoka sehemu na tabaka tofauti licha ya sera za Kikoloni za ‘wagawe uwatawale’ ambazo wakoloni walizieneza kote. Pamoja na hali hiyo, lakini yeye hakuweza kumbagua mtu kwa hadhi yake, kabila na wapi anatokea.” Amesema Aisha.

Anaeleza kuwa, akiwa mtoto wa kwanza wa Marehem Abdulwahid, katika miaka ya 1950 na 1960, alipata bahati ya kushuhudia ingia toka isiyokwisha ya msururu wa wageni, wakati mwingine wakifika katika nyakati za usiku.

Aisha, anasema katika ingia toka hiyo ya wageni nyumbani kwao, aliyeshika nafasi ya juu katika fikra zake akiwa mtoto,alikuwa ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,na kupitia kwake ndipo wakapata kujua kuwa kuna kabila linaitwa, ‘Wazanaki.’

 

Latest News

Most Read