Na Mohammed Abdul-Fattah Bayoumi

Mwenyezi Mungu (S.W.) amemtuma Mtume wake Mohammed (S.A.W.) kwa ajili ya rehma kwa walimwengu wote, ambapo Mwenyezi Mungu (S.W.) amesema: "Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote" Surat Al-Anbiyaa, aya 107

 

 Uislamu umewahimiza Waislamu wawe na rehma na huruma kwa viumbe vyote. Mtume (S.A.W.) amesisitiza maana hiyo kwa kusema: "Hakika Mwenyezi Mungu hawarehemu wasiowarehemu wanadamu" Bukhariy.

 Hivyo, wanadamu wote wanatakiwa kufanyiwa rehma bila ya kujali dini, rangi, kabila au kigezo chochote kingine, ambapo mojawapo ya misingi ya usamehevu wa dini hiyo adhimu, ni kuwarehemu wasio Waislamu na kuwatendea wema madhali hawawaudhi Waislamu wala hawawafanyii uadui.

Kwani, rehma ya Uislamu ni rehma ya jumla, siyo kwa watu maalumu wala kwa baadhi ya viumbe tu. Mtume (S.A.W.) amesema: "Kwa kweli Mwenyezi Mungu hamrehemu ila aliye warehemu wengine, Maswahaba wakasema: Ewe Mtume! Sote hivyo (tunawarehemu wengine), Mtume akasema: sikusudii mnavyofanya na wenzenu, bali na wanadamu wote" imesimuliwa na Abu Ya'ala na Al-Twabaraniy.

 Kwa hivyo, alama ya kwanza ya usamehevu katika Uislamu ni rehma ya kijumla, zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu (S.W.) amejiita Al-Rahmaan Al-Rahiim, ambapo majina haya mawili yanatokana na rehma, japokuwa Maulamaa wamekhitalifiana kuhusu tofauti iliyopo baina ya majina na sifa hizo mbili. Na namna lilivyo jina la Al-Rahiim linafungamana na waumini, wakati ambapo jina la Al-Rahmaan linahusiana na dunia nzima na hata akhera na viumbe vyote, basi rehma na huruma ni miongoni mwa sifa zake Mwenyezi Mungu (S.W.).

 Na kuwafanyia wema wasio Waislamu inamaanisha; kumfariji aliyepatwa na maafa kwa kutoa rambirambi akifiwa na mmoja wa jamaa wake, basi Muislamu anatakiwa kumfariji, maana wanadamu wote wanatakiwa kuhurumiana bila ya kujali mambo ya kuhitilafiana. Kwa hiyo, Waislamu wanatakiwa kuzingatia haki za majirani bila ya kutofautisha baina ya wale walio Waislamu na wale wasio Waislamu, kwani kuwafanyia majirani hisani na wema ni moja wapo ya alama za imani na ishara ya kukamilika imani kwa Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.

 Imesimuliwa kwamba "Abdullah bin Omar (R.A.) aliingia nyumbani kwake siku moja, akawakuta jamaa zake wamechinja (kondoo au mbuzi), akawauliza: Je, mmempa jirani yetu Myahudi sehemu kutoka nyama hiyo?! (Wakakaa kimya), akawauliza tena akiwa na ghadhabu kidogo: “Je, mmempa jirani yetu Myahudi sehemu kutoka katika nyama hiyo?” Kisha akawalaumu sana kwa kutompa jirani yao sehemu ya nyama japokuwa ni Myahudi".

 Kwa hivyo, tunaona kuwa Uislamu umewahimiza wafuasi wake wawe na matendo mema kwa wanadamu wote na hasa jirani hata wakiwa si Waislamu, kwa kuwatuza au kuwapa zawadi au chakula.

 Aidha, Mtume (S.A.W.) ametoa mifano bora kuwafanyia wasio Waislamu hisani na mema hata wakati wa vita, ambapo Mtume (S.A.W.) amewafundisha Maswahaba wake na Waislamu kwa jumla kuwa, usamehevu wa Uislamu lazima upatikane wakati wote na kwa wanadamu wote. Kwa hivyo, Mtume (S.A.W.) alipokuwa anapigana na washirikina na watu wa kitabu, aliwausia Maswahaba wake wawafanyie wananchi wa nchi zinazofunguliwa kwa wema hasa Wamisri, akisema: "Mkifungua Misri, wafanyieni watu wake wema kwani wana ahadi na jamaa baina yao na yetu". Imesimuliwa na Al-Haakim.

Na katika kitabu cha Sahihi Muslim: "Mtafungua nchi ambayo ina alama ya kutaja Qirat (aina ya sarafu), basi wafanyieni watu wake wema, kwa kuwa wana ahadi na jamaa inayowaunganisha nasi".

Imamu Al-Nawawy alisema kuna tamko jingine ambalo ni: "Mtafungua Misri, nchi inayotumia Qirat (sarafu), na mtakutana na watu wake ambao wana ahadi na jamaa baina yao na sisi, kwa hiyo wafanyieni mema wala msiwafanya ukatili".

Wanavyuoni wamehitilafiana kuhusu kuainisha maana ya Qirat katika hadithi zilizotajwa, wengi wamesema kuwa ni aina ya sarafu iliyokuwa inatumika nchini Misri, kama ni sehemu ya Dinar na Dirham na kwamba, Wamisri walikuwa wanaitumia sana sarafu hiyo katika miamala yao ya kila siku.

 Ama ahadi inayokusudiwa katika hadithi ni huruma na haki ya wanadamu, ambapo wamisri hawakuwa na ahadi baina yao na Mtume (S.A.W.) lakini amekusudia haki na huruma, na kuhusu jamaa ni kwa sababu ya kuwa Bi. Hajar, mama wake Nabii Ismail (A.S) ametoka Misri, pamoja na nasaba iliyopo kupitia Bi. Maria, mke wake Mtume (S.A.W.) ni mmisri pia.

 Tukiangalia usamehevu wa Mtume (S.A.W.) pamoja na Mayahudi unadhihirika wazi wazi katika misimamo mingi katika historia yake (S.A.W.). Miongoni mwa misimamo hiyo, siku moja Myahudi alimuua Swahaba mmoja katika mtaa mmoja wa Khaybar, Mayahudi wakaapa kuwa hawakumuua yule Swahaba wala hawajui ni nani aliyemuua, Mtume (S.A.W.) hakuwakadhibisha bali alikubali viapo vyao.

 Kwa mujibu wa aliyoyasimulia Bukhar kutoka kwa Bashir bin Yasar kwamba alisema: "Imetukia kuwa mmoja wa Answaar anayeitwa Sahl bin Abi Hathamaj, amemwambia kwamba kundi la Waislamu wa Answaar walikwenda Khaybar siku moja, wakamkuta Muislamu mmoja ameuawa, wakamtuhumu Myahudi mmoja kumuua mwenzao, Mayahudi wakasema: Hatukumuua wala hatujui ni nani aliyemuua”.

 Basi Maswahaba wakamjia Mtume (S.A.W.) wakasema: “Ewe Mtume! Tulikuwa Khaybar tukamkuta mwenzetu mmoja ameuawa huko”. Akasema Mtume: “Kwa kweli hili ni tukio kali mno, je, mnaweza kuleta dalili ya kuthibitisha ni nani hasa aliyemuua mwenzenu?” Wakasema: “Hatuna dalili”. Akasema: “Basi waape kwamba hawakumuua wala hawajui muuaji wake”. Maswahaba wakasema: “Hatukubali viapo vya Mayahudi kwani aghalabu wanasema uwongo wala hawana ahadi wala viapo”. Mtume (S.A.W.) akachukia kuacha damu ya yule Swahaba iwe bure, akatoa kwa jamaa zake ngamia mia moja kama ni fidia kutoka mali ya sadaka. La kuzingatiwa hapa ni kwamba Mtume (S.A.W.) alieleza kukubali viapo vya mayahudi.

 Vile vile, Mtume (S.A.W.) alikuwa anawatendea wema na usamehevu watu wote, hata wanafiki waliomuudhi sana, na hakuna dalili ya huruma yake (S.A.W.) na rehma yake kwa wanafiki hawa kuliko aliyoyafanya na Abdullah bin Ubay bin Saluul, aliyeongoza fitina ya kumshawishi jamaa wa Mtume (S.A.W.) katika tukio la Al-Ifk na kumtuhum Bi. Asha kwa unajisi na kuwasha fitina kubwa.

 Mwenyezi Mungu aliizima na kuahidi yule mkuu wa wanafiki na waliomfuata adhabu kali mno, japokuwa aliyafanya kumuudhi Mtume, Mtume (S.A.W.) alimfunika yule mnafiki kwa shati lake alipokufa, akaomba maghfirah kwake na kutangaza kuwa amemsamehe.

 Kwa mujibu wa aliyoisimulia Imamu Bukhar, mpaka kauli yake Mwenyezi Mungu (S.W.) imeteremshwa kubainisha kwamba, haifai kwa Mtume aombe maghfirah kwa watu hao na kwamba, hatima yao imeshapitishwa na Mwenyezi Mungu kwa waliyoyafanya duniani. "Waombee msamaha au usiwaombee. Hata ukiwaombea msamaha mara sabiini, Mwenyezi Mungu hatawasamehe" [Al-Tawbah: 80].

 Na wakati wa ufunguzi wa Makkah, usamehevu wa Mtume (S.A.W.) umedhihirika wazi, ambapo aliwapa Maqureish amani na usalama wao, japokuwa walimfanyia uadui wa kila aina na walimuudhi sana na kumlazimisha atoke nchini mwake, na aliporudi akiambatana na majeshi ya Waislamu wenye nguvu na ushindi hakuwafanyia washirikina uadui wala ukatili wowote, bali alisema:

 "Yeyote atakayeingia nyumba ya Abu Sufyan, basi yuko salama, na yeyote atakayekaa nyumbani mwake hataudhiwa, na yeyote atakayetupa silaha yake, basi hatapiganiwa". Kisha akawaachilia huru mateka wote. Imesimuliwa na Muslim.

 Pia, Mtume (S.A.W.) kwa mijibu wa rehma yake na usamehevu wake hakuwa anawazuia waumini wawsiliane na jamaa zao ambao bado wapo ushirikina, Imamu Bukhariy amesimulia kuwa Bi Asmaa bint Abi Bakar (R.A.) alisema: "Mamangu bado hajasilimu, nikamwuliza Mtume (S.A.W.) Je, naruhusiwa kuwasiliana naye?! Akasema: Ndiyo".

Hivyo, Mtume (S.A.W.) alikuwa rehma kwa walimwengu wote Waislamu na wasio Waislamu, na rehma yake hiyo ilikuwa na ishara kadhaa za upendo, usamehevu, msamaha na kuusiana mema na kwamba, matini nyingi za Qur’ani Tukufu na Sunna Takatifu ya Mtume (S.A.W.) zilithibitisha hivyo na kuelezea hali yake Mtume (S.A.W.) katika awamu zote za maisha yake, kupitia vitendo vyake na mwenendo wake, kuamiliana na Waislamu na wasio Waislamu ambapo misemo na vitendo na hali zake zote, zilikutana kusisitiza kuwa yeye ndiye mfano bora wa rehma kwa dunia nzima na maisha yote katika nyanja zake mbalimbali.  

Email : This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it._center