Na Said Rajab

Wakati tunapoondoka hapa duniani kwenda ulimwengu mwingine, inakuwa kama safari ya ndege kutoka nchi moja kwenda nyingine. Nchi ambayo maelezo yake hayawezi kupatikana kwenye

majarida yanayovutia ya safari za anga, isipokuwa ndani ya Qur'an na Hadithi za Mtume wa Mwenyezi Mungu. Nchi ambayo usafiri wetu kwenda huko, hautakuwa wa mashirika ya ndege ya Air Tanzania, Kenya Airways, British Airways, KLM, Gulf Air au Emirates bali ni 'Air Janazah'!!

'Shirika la ndege' ambalo mizigo yetu ya kuingia nayo kwenye ndege, haitakuwa zile kilogramu 30 zinazoruhusiwa, isipokuwa amali zetu hata zikiwa na uzito wa kiasi gani.

Kule hatulipii uzito uliozidi wa mizigo yetu (excess luggage). Mizigo yote inabebwa bila ya malipo, kwa hisani ya Muumba wako.

Na nguo zetu hazitakuwa za thamani na gharama kubwa kama suti za 'Pierre Cardin' au zinazofanana na hizo, bali shuka moja tu nyeupe ya pamba. Na manukato yako ni karafuu maiti.

Kwenye usafiri huu, pasi zetu za kusafiria hazitakuwa za Tanzania, Kenya, Uingereza, Ufaransa au Marekani, bali Uislamu. Viza zetu hazitakuwa za miezi sita, mwaka, za masomo, za kutalii au nyinginezo isipokuwa "La Illaha Illallah".

Katika usafiri huu, wahudumu wa ndani ya ndege (air hostess) siyo wasichana warembo, bali Israili na malaika wengine wa Mwenyezi Mungu. Huduma za ndani ya ndege hiyo hazitakuwa daraja la kwanza au 'economy' bali kipande cha nguo kilichowekwa marashi yanayonukia au yasiyonukia vizuri. Na mahali tunapokwenda (destination) hakutakuwa 'Heathrow Terminal 1', au 'Jeddah International Terminal' bali 'Terminal Graveyard' (makaburini).

 Maeneo yetu ya kusubiri (waiting lounge), hayatakuwa vyumba vilivyonakshiwa mazulia ya kupendeza na vilivyowekwa viyoyozi, bali shimo linalotisha la futi sita. Maafisa  Uhamiaji hawatakuwa wa Serikali, bali 'Munkar' na  'Nakir'. Wao wanaangalia tu kama unastahili kwenda mahali unapong'ang'ania. Hakuna haja ya maafisa wa Forodha kule wala vifaa vya kubaini wakwepa kodi na ushuru.

Uwanja wa ndege wa kuunganishia safari hii (transit airport) utakuwa Al Barzakh, ambapo kituo chetu cha mwisho (final destination) kitakuwa ama Bustani ambazo chini yake kunatiririka maji au moto wa Jehanamu.

Ndugu zangu katika Imani, safari hii haina gharama yoyote, ni bure kabisa, kwa hiyo fedha zote ulizoweka akiba hazitakusaidia. Ndege hii kamwe haiwezi kutekwa wala kulipuliwa, kwa hiyo usiwe na wasiwasi kuhusu magaidi.

Hakutakuwa na huduma ya chakula ndani ya ndege hii, kwa hiyo usiwe na wasiwasi kuhusu 'allergy' zako au kama chakula kitakuwa halal au la. Usiwe na wasiwasi kuhusu mahali pa kunyoosha miguu yako ukiwa umekaa kwenye siti, kwa sababu miguu yako itakuwa haina kazi tena.

Na wala usiwe na wasiwasi kuhusu kuchelewa. Ndege hii huwa haichelewi kamwe, na wakati wote inazingatia muda. Inakuja na kuondoka kwa wakati ule ule uliopangwa.

Usiwe na wasiwasi pia kuhusu programu za burudani ndani ya ndege hii, kwa sababu utakuwa umepoteza hisia zote za furaha unapoingia tu. Huna haja ya kufanya 'booking' ya safari hii, tayari 'booking' imeshafanywa (return) tangu siku ile ulipokuwa mimba ndani ya tumbo la mama yako.

Ah! hatimaye habari njema! Usihofu nani atakayekaa jirani na wewe. Utakuwa na raha ya kuwa abiria pekee ndani ya ndege hii. Kwa hiyo furahia safari hii kadri unavyoweza. Kama unaweza! Hata hivyo, tahadhari moja ndogo, safari hii huwa haina taarifa.

Je? Umeshajiandaa kwa safari hii, ambayo lazima itakuja?? Ndugu yangu katika Imani afadhali ufanye hivyo!