Na Bint Ally Ahmed

NI watu wachache sana katika jamii ambao huwa na moyo wa kijasiri wa kukataa kuwa tegemezi kutokana na mapungufu ya kimaumbile hususani kuwa

katika ulemavu fulani wa viungo na kuamua kujishughulisha kwa namna yoyote na kuweza kujiingizia kipato.

Bi. FATUMA  Amri  Abdallah, ni miongoni mwa watu hao. Ni binti aliyezaliwa mwaka 1981, Mkoani  Mtwara na ni mlemavu wa miguu aliyejitolea kufanya kazi  kwa nguvu zake na kukataa kuwa ombaomba pamoja na ulemavu alionao.

Bi. Fatuma, ni mlemavu wa miguu yote miwili. Ili atoke sehemu moja kwenda sehemu nyingine, ni lazima atambae. Lakini pamoja na kuwa katika hali hiyo, amejaliwa kuwa na mume na mtoto mmoja. Kwake hili ni jambo la kushukuru pia.

Pamoja na kuwa katika ndoa akiwa mlemavu wa miguu, hali hiyo haijamfanya abweteke. Ameamua kujishughulisha na utafutaji wa riziki. Bi. Fatuma ni dereva wa usafiri maarufu Jijini Dar es Salaam wa Pikipiki za miguu mitatu, maarufu kama Bajaji.

Bi. Fatuma, amejitosa kufanya shughuli hiyo ya usafirishaji katika Mtaa wa Kongo na Uhuru Kariakoo Jijini Dar es Salaam, mtaa wenye kila aina ya vurugu, msongamano wa watu na magari. Anafanya safari kutoka mtaa wa Kongo kwenda Ferry na cha kuvutia Zaidi, kazi hiyo anaifanya huku akiwa katika vazi sahihi la hijabu (ndani ya Nikaab).

Ukimuona Bi. Fatuma, akiwa  katika kazi yake ya kuendesha Bajaji, huwezi amini jinsi alivyojistiri kuanzia kichwani mpaka kwenye unyayo na huwezi kuona sehemu ya mwili wake,  labda sehemu ndogo ya macho yake na huwezi kujua kama ni mlemavu wa miguu.

Bi. Fatuma amesema, yeye ni mlemavu lakini hakutaka kukaa nyumbani na kuanza kuwa omba omba kama ambavyo tumezoea kuwaona baadhi ya watu wenye ulemavu kama yeye.

Anasema, katika familia yao yeye pekee ndio mwenye ulemavu. Hata hivyo hakuzaliwa mlemavu, bali alipata ulemavu akiwa na umri wa miaka mitatu, baada ya kuugua na kupelekea ulemavu huo lakini kabla ya hapo  alikuwa anatembea kwa miguu yake kama kawaida.

Hakuanza na kazi aliyonayo sasa, bali kabla ya hapo alipomaliza Shule ya msingi, Mkoani Mtwara alianza kujishughulisha na kupika maandazi, chapati na vitumbua. Anasema, baadae alipata hamu ya kuondoka Mkoani Mtwara na kuja Jijini Dar es Salaam.

Lakini alipomueleza mama yake mzazi nia yake hiyo, anasema mama alikataa na hakumpa sababu ya kumkatalia. Ila anadhani mama yake alikuwa akihofia kuwa mwanae atajiingiza katika kazi ya kuomba. Hata hivyo Bi. Fatuma, alimhakikishai mama yake kuwa hatojiingiza katika shughuli ya kuwa ombaomba kwa ulemavu wake.

Bi. Fatuma, anasema alimjengea hoja mama yake kuwa yeye ana ulemavu wa miguu lakini Mwenyezi Mungu amemuachia akili na mikono katika hali ya utimamu wake hivyo anaweza kujishughulisha na kazi mbalimbali na kuweza kujipatia kipato halali.

Hatimae aliingia Jijini Dar es Salaam, akitokea Mtwara na kufikia kwa kaka yake anaeishi Yombo Buza, na baada ya muda alimuomba kaka yake mtaji ili aanze kujishughulisha na  biashara ndogo ndogo.

Alipata mtaji kutoka kwa kaka yake ambapo alianza kuuza saa na mikoba ya wanawake, sehemu ama kituo chake cha kwanza kufanyia biashara hizo kikiwa pale Karume Jijini Dar es Salaam.

Anasema, siku moja alienda kuswali Msikiti wa Lindi, Kariakoo Jijini Dar es Salaam, wakati huo alikuwa akitumia Baiskeli  za walemavu ambayo pia ilikuwa ikimsaidia kubeba bidhaa zake za biashara. Bi. Fatuma, anasema aliacha mzigo wake nje katika baiskeli yake na kuingia Msikiti, kwa ajili ya kufanya ibada  lakini alipotoka hakuukuta mzigo. Yaania aliibiwa mzigo wote wa biashara zake.

Pamoja na mtihani huo aliopata hakukata taama. Hali hiyo ilimsukuma kwenda kwa jamaa mmoja wa Kihindi na kumueleza tatizo lake ambapo aliulizwa kama ataweza kazi ya kuendesha Pikipiki aina ya Bajaji.

Bila hofu na kwa kujiamini Bi. Fatuma, alijibu kuwa ataweza na kwamba yupo tayari kufanya kazi hiyo. Hata suala la kuwa na leseni lilikuwa kama ni dalili ya kikwazo kwake kupata neema ya kazi hiyo, iliyomsukuma kwenda kujiunga na Chuo cha Ufundi, Polisi Kilwa Barabara ya Kilwa na kusomea udereva na baada ya kuhitimu alipata leseni ya kumhalalisha kufanya kazi ya udereva barabarani kwa mujibu wa sheria.

Baada ya kuhitimu kozi hiyo ya udereva na kurudi kwa Mhindi, Bwana huyo aliamua kumnunulia Pikipiki ya miguu mitatu aina ya Bajaji na kusaini mkataba kwa makubaliano maalum ya kibishara.

Bi. Fatuma, amewataka wanawake wasiogope kufanya kazi wakiwa katika stara, kwani kazi ni za muda mchache lakini Stara ndio kila kitu.

“Kumbuka utaenda kujibu nini mbele ya Allah kwa kuacha stara kwa ajili ya kazi, ikibidi ifike mahala mwanamke uwe tayari kuacha kazi kwa ajili ya kuzuiwa kuwa katika stara, kwani rizki anatoa Allah.” Anasema Bi Fatma akiwaasa wanawake wenzake.

Anasema, wakati anaanza kazi yake ya udereva, alitakiwa na Askari wa barabarani kuvua Nikabu kwa maelezo kuwa haifai kuendesha chombo cha moto akiwa amevaa vazi hilo. Hata hivyo aliwaeleza kuwa yupo tayari kuacha kazi, lakini sio kuvua vazi lake.

Anasema, alisimamia hoja yake.

Anasema, changamoto nyingine ilikuwa ni kutoka kwa abiria kwani wengi walikuwa wakiikwepa Bajaji yake wakihofia uvaaji wake, wengine wakimfanyia kila aina ya kebehi.

Lakini anasema alibakia na msimamo wake na walio panda aliwapa huduma yake vizuri na kupata riziki yake na kadri siku zilivyozidi kwenda, abiria walijenga imani naye na kwa sasa amekuwa na wateja wengi wakipanda chombo chake bila hofu kwa kuwa wameshamzoea.

Kupitia kazi hiyo mpaka sasa Bi. Fatuma, anaweza kumsomesha mwanae na kumiliki kiwanja ambapo tamaa na malengo yake ni kujenga nyumba. Hata hivyo akasema, sio vibaya kama Waislamu watamuunga mkono kwa kumsadia vifaa vya ujenzi kama vile matofali, sementi na mbao. Bi. Fatuma, anapatikana kupitia namba  za simu:-0719 319 348.

 

 

 

 

 

Most Read

  • Week

  • Month

  • All