Zanzibar ina Wabunge zaidi ya 50 katika Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Kati ya wabunge wote hao wanaotoka vyama vya CCM na CUF

kuna wachache mno ambao wana mchango na msaada wa maana kwa Zanzibar. Bila ya kuegemea katika siasa za vyama, nathubutu kusema kwamba wabunge wengi wanaotoka Zanzibar wa vyama vyote, hawaoneshi uwezo unaostahiki katika utendaji wa kazi zao.

Siasa za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zimewajenga watu kuamini zaidi katika vyama vya siasa badala ya kuamini hali halisi iliyomo ndani ya vyama husika. Hali hii inatafautiana sana na mwenendo wa kisiasa katika nchi zilizoendelea hasa za Ulaya ya Magharibi na Marekani. Wenzetu huweka pembeni siasa za vyama hasa inapotokezea mambo muhimu ya nchi kukwama. Kwa mfano Ufaransa kuna ‘harakati’ iliyoibuka hivi karibuni inayoitwa kwa Kifaransa “ Gilets Jaunes” yaani Vizibao vya Manjano kwa lugha ya Kiswahili. Kundi hili halifungamani na siasa za chama chochote na limeibuka na madai mbali mbali ambayo mengi yao hakuna chama cha siasa kilichowahi kuyadai hapo awali. Ni wazi kwamba baadhi ya wafuasi wa kundi hili ni watu kutoka vyama tafauti vya siasa, lakini wameweka pembeni misimamo ya vyama vyao na kuwa na kauli moja.

Nimetowa mfano wa gilets jaunes kuwatanabahisha Vijana na Wananchi wa Zanzibar kwamba linapokuja suala gumu na la maslaha ya nchi, si busara kufuata misimamo ya kichama. Wananchi wanapoungana wakawa kitu kimoja, vyama vya siasa vitawajibika kuwafuata (wananchi) badala ya wao (wananchi) kuburuzwa na misimamo ya vyama vyao. Kwa msingi huu, tayari imefika wakati kwa wanachama wa vyama vya CUF na CCM kupinga baadhi ya mambo ambayo hayaendani na maslaha mapana ya Zanzibar.

Kuna mtaalamu anayesema kwamba “L’homme élu l’homme perdu” ikimaanisha kwa Kiingereza “ An elected man is a lost man”. Katika siasa mara nyingi ukimchaguwa mtu huwa hakujuwi wala kukumbuka tena. Huona kwamba yeye ndo keshachaguliwa kuwa bwana mkubwa na kuwaona wenzake wote hawana maana. Kauli hii ya Mtaalam wa siasa wa Ufaransa inathibitishwa kwa vitendo na mienendo ya wabunge walio wengi kutoka Zanzibar yaani Unguja na Pemba na kutoka vyama vyote vya CCM na CUF. Wabunge wengi kutoka Zanzibar wanaonesha kujali zaidi maslahi binafsi na vyama vyao kuliko maslahi mapana ya wananchi waliowatuma. Hapo ndo tunaposema kwamba kama Zanzibar ingekuwa na Wabunge 10 tu wenye kujali maslahi ya wananchi na kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya upembuzi na kujenga hoja kwenye mambo ya msingi yanayouhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, naamini hata haya mazonge ya Muungano tuliyonayo yangekwisha punguwa kwa kiasi kikubwa ama kumalizika kabisa. Msamiati “Kero za Muungano” ungekuwa historia.

Kwenye hili la wabunge, binafsi nawagawa Wabunge wetu katika makundi makuu manne:

Kundi la kwanza ni la wabunge wenye uwezo mkubwa wa kitaaluma na kiutendaji na ambao wamejitolea katika kuhakikisha maslahi mapana ya Wananchi. Wabunge hawa ni wachache mno na wamo katika vyama vyote vikuu kwa Zanzibar yaani CUF na CCM.

Kundi la pili ni la Wabunge wenye uwezo mkubwa wa kitaaluma, lakini limekumbwa na watu wenye kujali maslahi binafsi na wavivu. Hawajishughulishi kufanya rejea zitakazowawezesha kujenga hoja madhubuti juu ya mambo mbali mbali yanayoisibu Zanzibar. Ubinafsi na uvivu wa wabunge wa kundi hili umewafanya wabunge hawa waonekane kuwa na uwezo mdogo wa kiutendaji. Hawa wakipata shinikizo kutoka kwa wananchi waliowachaguwa ama vyama wanavyoviwakilisha wanaweza kubadilika na kufanya kazi nzuri kabisa itakayosaidia kutatua kero mbali mbali zinazowakabili wananchi.

Kundi la tatu ni lile la Wabunge waliochaguliwa ama kuteuliwa kwa kushiriki sana katika shughuli za kijamii kama vile harusi na maziko lakini kiukweli hawana uwezo wa kitaaluma wala wa kufanya kazi za kibunge. Uzuri wa wabunge wa kundi hili ni kwamba japokuwa wamekosa taaluma, bado wana mapenzi ya kweli na wananchi wao. Wao wapo kutetea maslahi mapana ya Zanzibar na wananchi wake lakini kutokana na ufinyu wa kitaaluma na kiutendaji, wanashindwa kuzipanga vizuri hoja zao, hivyo mara nyingi hushindwa kufikia lengo. Kundi hili hata likilaumiwa si rahisi kubadilika kwa sababu halina uwezo unaohitajika kitaaluma na kiutendaji.

Kundi la mwisho, ni lile linalojumuisha wabunge ambao wana sifa za wabunge wa kundi la tatu katika kuchaguliwa kwao, hawana taaluma wala uwezo wa kiutendaji. Kilichoongezeka kwa wabunge wa kundi hili ni kwamba mbali ya kukosa taaluma na uwezo wa kiutendaji bado pia wametumbukia kwenye kujali maslahi binafsi. Kwa muono wangu wabunge wa kundi hili ndio wabaya zaidi kuliko makundi matatu yaliyoelezwa juu.

Mwisho, labda nitowe rai kwa Wananchi kutafuta watu makini wa kuwapendekeza kugombea nafasi tafauti. Kadhalika, kuwe na utaratibu maalumu wa kuwachunguza wagombea kitaaluma, kiutendaji na kikhulka.

Ikumbukwe kwamba kuna wabunge wenye taaluma lakini wavivu katika kazi jambo ambalo huwafanya wasiwe na uwezo wa kiutendaji. Pia kuna wabunge waliosoma lakini hubabaika kwa mambo madogo tu na kuwasahahu mpaka wananchi waliowapandisha ngazi wakafika huko Bungeni.

Wananchi amkeni kwani uwepo wa viongozi wabovu ni ishara ya kuwepo kwa wananchi wabovu.

Mohamed Juma Abdalla 02 Febuari,2019 Zanzibar.

 

Latest News

Most Read

  • Week

  • Month

  • All