Rais Mwinyi, ACT mmepatia

 

Othman Masoud Othman, ndiye Makamu wa Kwanza rais Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Hassan Mwinyi, amemteua na kumwapisha kuchukua nafasi ya marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, aliyefariki tarehe 17 Februari mwaka huu.

Mh. Othman Masoud, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, aliwahi kuwa Mwendesha Mashitaka Mkuu wakati wa utawala wa Rais Amani Karume na kisha kuwa Mwanasheria Mkuu kwenye utawala wa Rais mstaafu Ali Mohamed Shein.

Uteuzi wa Masoud, umefanywa na Rais wa Zanzibar, Dkt Hussein Mwinyi baada ya mashauriano na chama cha ACT-Wazalendo.

Wengi wanamfahamu, sura yake si ngeni katika siasa, maana tangu aondolewe ndani ya SMZ, alikuwa maarufu kwa misimamo yake ya kutetea maslahi ya Zanzibar katika Muungano.

Tunavyofahamu, Mh. Masoud, Ismail Jusa na Babu Juma Duni, walikuwa ni miongoni mwa majina yaliyokuwa yakitajwa mitandaoni baada ya chama cha ACT kutangaza kuwa wamepeleka jina kwa Rais Mwinyi kwa ajili ya uteuzi.

Ni mpole azungumzapo, lakini kwa ndani ana msimamo usioyumba kwa yale anayoamini ni ya maslahi kwa Zanzibar. Na pia haogopi kuyasema yale yasiyo na maslahi kwa visiwa hivyo.

Kwa kuzingatia haiba, wasifu, uchapakazi, uzalendo na misimamo yake ya kizalendo inayoegemea maslahi ya Wazanzibar, tuseme tu kwamba Rais Mwinyi na ACT hawajakosea.

Tunaamini sifa hizo ndizo zilizomfanya kuwa maarufu katika medani ya siasa za visiwani kiasi cha kufikia kuteuliwa kuwa mjumbe katika kamati ya ilani ya chama cha ACT Wazalendo, kabla ya jina lake kupendekezwa kuwa mrithi wa Maalim Seif.

Kwa taaluma yake ya sheria na uwezo mzuri wa kuuchambua masuala ya uongozi na muungano, uwepo wake katika SMZ, hakika umesaidia sana kupatikana ufumbuzi wa baadhi ya zile kero za miaka mingi za muungano wa nusu karne sasa.

Katika mahojiano yake ya kwanza na chombo kimoja cha habari tangu atangazwe kuwa Makamu wa Kwaza wa Rais, Mh. Othman amenukuliwa akisema,"Zanzibar inastahili kuwa inapotakiwa kuwa, sio hapa ilipo sasa. Kulihitajika mashirikiano na uongozi bora. Kwa sasa kuna fursa ya aina yake kulifanikisha hilo."

Lakini tutakuwa wachoyo wa fadhila iwapo hatutampa heshima yake Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, kukubali Mh. Othmani kuwa Makamu wake wa Kwanza.

Tunampa heko kwa kuwa tunaamini kabisa kwamba, kitendo chake cha kumkubali bila kusita Mh. Othman kuwa Makamu wake wa Rais, ameangazia zaidi uwezo wake na maslahi ya Wazanzibar kuliko maslahi ya siasa za vyama.

Tunasema hivyo kwa kuwa tunaamini kabisa kwamba Rais Mwinyi anamfahamu vizuri Mh. Othman, juu ya dhamira yake na misimamo yake kwa Wazanzibar.

Rais Mwinyi anaufahamu msimamo na rekodi za Mh. Othman Masoud katika utendaji na katika siasa, ameashiria kuwa na mtazamo sawa na mtangulizi wake Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, hasa kuhusiana na uwepo wa fikra za umoja wa Wazanzibari na maendeleo ya visiwa hivyo. Fikra ambazo bila shaka zinaafikiana na aina ya uongozi wa Dkt. Hussein Mwinyi.

Wanaomfahamu Mh. Othmani, wataafikiana nasi kwamba hakuwa na historia katika majukwaa ya kisiasa. Hata siasa za upinzani hakuwa mshiriki wa wazi. Kwa maneno mafupi hajawahi kudhihirisha uwezo wake katika majukwaa ya kisiasa mbali yakutumia taaluma yake kuitetea Zanzibar.

Maalim Seif alikuwa mwanasiasa. Kaiogelea bahari hiyo tangu akiwa kijana mbichi. Kapita katika vyama kadhaa vya kisiasa, kuanzia chama tawala CCM, Chama cha Wananchi (CUF), hatimaye ACT Wazalendo.

Hoja kwamba Othman hana mizizi ya kisiasa, haiwezi kuwa kigezo cha kumfanya asiwe mrithi mzuri wa Maalim. Hoja hiyo inaonesha tu ile tofauti ya Maalim na Othman katika muktadha wa historia zao.

Tuseme tu kwamba Mh. Othman kiutendaji ni chaguo bora kuliko kisiasa na tunaamini atakuwa Makamu bora kabisa wa Rais kwa maslahi ya Wazanzibar.

Rais Mwinyi kapata msaidizi bora wa zama zake, ACT wamepatia hasa kwa kuzingatia mustakabali wa mwaka 2025 na Wazanzibar watanufaika zaidi. Hatuna shaka, Othman amekidhi kama si zaidi.

Tunafahamu Rais Mwinyi hakuwa mahiri sana kwenye majukwaa ya kisiasa, lakini alikuwa mahiri zaidi kiutendaji. Tunaweza kusema, hawa wamepatana.

Tunaamini miaka yao mitano ya uongozi wa serikali ya Zanzibar, watadhihirisha kwa matokeo chanya juu ya uwezo wao wa kisiasa na kuiongozi na kuwafuta Wazanzibar machozi ya kuondoka Maalim Seif.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Latest News