Mwanasiasa wa mrengo wa kulia na Mbunge wa zamani nchini Uholanzi, Joram van Klaveren, ambaye alikuwa na chuki kubwa dhidi ya Uislamu, ameibua gumzo nchini humo baada ya kutangaza kubadilisha msimamo wake na kusilimu.

Kwa muda wa miaka saba Van Klaveren, aliongoza kampeni ya kuupinga Uislamu katika Bunge la Uholanzi akiwa katika chama cha Freedom Party (PVV), cha mwanasiasa Geert Wilders, ambaye ni maarufu kwa chuki zake dhidi ya Uislamu.

Akiwa bungeni, Van Klaveren alitaka niqabu ipigwe marufuku na pia alitaka minara ya Misikiti isijengwe nchini humo, huku akisisitiza kuwa nembo zote za Uislamu zinapaswa kupunguzwa Uholanzi.

Lakini sasa Van Klaveren, (40) amenukuliwa akiliambia gazeti la NRC kuwa, wakati akiwa katika utafiti wake wa kuandika kitabu dhidi ya Uislamu, alibadilisha fikra yake na sasa kitabu chake kinakabiliana na nadharia za wanaoupinga Uislamu.

Amenukuliwa akisema, "Sasa mimi ni Muislamu.

Taarifa zinasema Van Klaveren, alisilimu na kuukubali Uislamu katika maisha yake mnamo Oktoba 26 mwaka 2018, hatua ambayo iliwashangaza marafiki na maadui wake.

Van Klaveren alijitenga na Wilders mwaka 2014 kutokana na matamshi ya kiongozi huo wa Freedom Party, ambaye aliwachochea Waholanzi wawatimue watu wenye asili ya Morocco.

Van Klaveren aliunda chama kipya alichokiita "For Netherlands” (VNL), lakini alistaafu katika siasa baada ya kushindwa kushinda kiti katika uchaguzi wa mwaka 2017.

Said Bouharrou wa Baraza la Misikiti ya Wamorocco Uholanzi amempongeza Van Klaveren na kusema ni hatua kubwa kwa mtu ambaye alikuwa mpinzani mkubwa wa Uislamu kutambua haki na kuongeza kuwa ni ujasiri pia kwake kutangaza uamuzi wake hadharani. (IQNA).

 

Most Read

  • Week

  • Month

  • All