Baraza UN walaani mpango wa Israel kutwaa ardhi ya Palestina

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limelaani mpango wa utawala wa Kiayuni wa Israel wa kutwaa na kughusubu ardhi ya Palestina ya Ukanda wa Ghaza.

Katika kikao chake cha 43, Baraza la Haki za Binadamu la UN sambamba na kulaani uamuzi wa utawala dhalimu wa Israel wa kukalia na kutwaa asilimia 30 ya eneo la Ukingo wa Magharibi, limeitaka Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu kutayarisha ripoti kuhusu athari mbaya za uamuzi huo.

Baraza hilo pia limepasisha azimio lililopewa jina la "Azimio la Vitongoji" linalotoa wito wa kususiwa bidhaa zinazozalishwa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Azimio hilo ambalo hupasishwa kila mwaka katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, pia limetahadharisha kwamba watu wanaojihusisha na biashara katika maeneo hayo pia wanapaswa kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Baraza hilo pia limepitisha maazimio mengine manne dhidi ya Israel, likiwemo lile linalolaani hatua ya utawala huo haramu ya kulikalia kwa mabavu eneo la Miinuko ya Golan ya Syria.

Aprili mwaka huu Waziri Mkuu Netanyahu na Gantz walikubaliana kutwaa asilimia 30 ya eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi na kuliunganisha na ardhi nyingine zilizoghusubiwa za Palestina ifikapo mwezi Julai mwaka huu wa 2020. Parstoday.