Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amesema kuwa, utovu wa kimaadili na kashfa za ngono za baadhi ya Makasisi wa Kanisa hilo ni maafa na akakiri juu ya kutumiwa vibaya kijinsia wanawake katika Makanisa ya Katoliki.

Papa Francis ameashiria kashfa za ngono na ubakaji wanawake unaofanywa na baadhi ya Makasisi wa Kanisa Katoliki na kusema kuwa, hakubaliani na mapendekezo ya makundi yanayotetea uhuru na haki za wanawake, likiwemo la mwanamke kuchaguliwa kushika nafasi ya juu kabisa ya uongozi wa kidini.

Amesema kuwa, Kanisa Katoliki linapaswa kuzingatia madai ya kisheria ya watu wanaopigania uadilifu na usawa.

Hivi karibuni, Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani alitangaza rasmi sheria inayopiga marufuku kuwatumia vibaya kijinsia watoto wadogo katika makao Makuu ya Kanisa hilo- Vatican, na maeneo mengine yanayofungamana na Kanisa hilo duniani kote.

 Mwaka uliopita wa 2018, Kanisa Katoliki lilikumbwa na kashfa nyingi za kingono zilizowahusisha Makasisi katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Chile, Marekani, Ujerumani na Australia.

Kashfa hizo ziliibua lawama kali duniani dhidi ya Vatican na Papa Francis mwenyewe.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki alituhumiwa kuficha ufisadi mkubwa wa kingono ndani ya Kanisa hilo, hasa kwa kuzingatia kwamba, mara baada ya kushika wadhifa huo alimteua Kasisi mmoja aliyekuwa akituhumiwa kuhusika na vitendo vya liwati kuwa mshauri wake wa ngazi za juu.parstoday.