Katika kile kinachoonekana ni mwendelezo wa ukiukaji wa haki za kiraia za msingi za Wamarekani wenye asili ya Afrika, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali katika wilaya ya Sacramento jimboni California, imewaondolea mashitaka maafisa wa Polisi waliommiminia risasi na kumuua kijana Mweusi ambaye hakuwa amejizatiti kwa silaha yoyote mwaka jana.

Mwendesha Mashitaka Mkuu wa eneo hilo, Anne Marie Schub, Jumamosi ya wiki iliyopita alitoa taarifa inayohalalisha mauaji ya kijana huyo kwa jina Stephen Clark, aliyekuwa na umri wa miaka 22 mnamo Machi mwaka jana.

Alisema, "Lazima tufahamu kuwa maafisa wa polisi hulazimika kufanya maamuzi ndani ya sekunde chache, na lazima pia ifahamike pia kuwa wanafanya kazi katika mazingira ya taharuki."

Hii ni katika hali ambayo, mashahidi na mawakili wa kijana huyo aliyeuawa, wanasema kuwa Clark alipigwa risasi na maafisa wawili wa Polisi wa Sacramento waliyedhani kuwa amebeba bastola, katika hali ambayo alikuwa amebeba simu ya mkononi.

Visa vya ukatili wa polisi wa Marekani dhidi ya raia wa nchi hiyo wenye asili ya Afrika vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara nchini humo.

Septemba mwaka jana, Joshua Harvey, kijana Mmarekani Mweusi aliyekuwa na umri wa miaka 25 alipoteza maisha baada ya kushambuliwa mara kadhaa kwa kutumia shoti ya umeme na Polisi wa mji wa Tulsa, katika jimbo la Oklahoma nchini humo. Parstoday.