Na Bakari Mwakangwale

SHURA ya Maimamu Tanzania, imesema Waislamu watatoa msimamo wao hivi karibuni kufatia azima ya Jeshi la Polisi, kutaka kuingilia mafundisho ya Uislamu katika Madrasa na Shule za Kiislamu.

SHURA ya Maimamu Tanzania, imesema Waislamu watatoa msimamo wao hivi karibuni kufatia azima ya Jeshi la Polisi, kutaka kuingilia mafundisho ya Uislamu katika Madrasa na Shule za Kiislamu.

Kaimu Amir wa Shura ya Maimam Sheikh Shaaban Ibrahim, ameyasema hayo akiongea na gazeti la An nuur, kuhusu kauli ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Siro, aliyesema kuwa wataanza kukagua mafunzo yanayotolewa katika Madrasa na Shule za Jumapili (Sunday Schools).

Hata hivyo Kamanda Siro, alisema watawashirikisha Mapdri, Maaskofu na Masheikh kwa upande wa viongozi wa Dini na kwa upande wa Jeshi la Polisi, watashirkisha timu ya kupambana na makosa ya kigaidi.

Kamanda Siro alisema, lengo ni kupitia Silabi na mafunzo yanayotolewa katika Madrasa na Shule za Jumapili (Sunday School), Shule za Sekondari mpaka vyuoni ili kuona yanayofundishwa na viongozi wa Dini ni kwa ajili ya kuwajenga vijana wa Kitanzania katika uzalendo au ni kwa ajili ya kuwabomoa.

Amir Ibrahim, ambaye pia ni Imamu Mkuu wa Msikiti wa Tungi Temeke, amesema katika hatua za awali tayari Maimamu chini ya Shura ya Maimamu, wamekutana, pamoja na mambo mengine lakini pia wamejadili kauli ya IGP Sirio, na kuazimia kiandaliwe kikao kitakacho jumuisha Jumuiya na Taasisi za Kiislamu.

“Kikao hicho kitakuwa na uwakilishi wa Waislamu kutoka Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, watajadili suala hilo kisha kwa pamoja watatoa kauli na kueleza msimamo wa Waislamu kuhusu azima ya Jeshi la Polisi, kuingilia mafundisho ya Uislamu katika Madrasa na Shule za Kiislamu.” Amesema Amir Ibrahim.

Amir Ibrahim, alisema katika kiko chao cha awali walichokutana wameona kwamba kauli ya Kamanda Siro, ni kama inakwenda kinyume na Katiba ya Nchi, kwa sababu hayo anayotaka kuyafanya ni kuingilia masuala ya kiimani na kwa Waislamu Elimu ni ibada.

Alisema Jeshi la Polisi, haliwezi kukosoa au kuingilia masuala ya kiimani kwani wenye mafundisho yao ndio wenye tafsiri sahihi ya kinachofundishwa ambapo kwa Waislamu mafundisho yao yanazingatia Qur an na Sunnah ya Mtume (s.a.w).

“Waislamu wanaamini kuwa kusoma ni Faradhi, tunapomfundisha mtoto kusoma Elimu, tayari tupo kwenye ibada na anachofundishwa ni kile kilichopo katika Qur an na sunna za Mtume (s a w), Fiqi anayofundishwa iwe Madrasa, Shuleni au Chuoni imechimbuliwa katika Qur an na Sunnah za Mtume.”

“Sasa kufika mahala kuonyesha mashaka kwa hayo mafundisho na kutaka yachunguzwe kwa dhana kuwa mafundisho hayo hayafundishi uzalendo au yanaharibu vijana hii ni kashfa kubwa kwetu sisi Waislamu.” Amesema Amir Ibrahim.

Alisema, ikumbukwe kuwa viongozi wa Serikali huwahimiza viongozi wa Dini, kuwajenga waumini wao katika maadili kwa sababu Mtanzania mzuri ni yule aliyepata maadili mema, sasa Kamanda wa Polisi, anaposema huenda mafundisho ya dini ndiyo yanayoleta uhalifu, hiyo ni kashfa.

Kamanda Siro, alisema katika ufatilia wa mafundisho hayo watashirikisha timu ya kupambana na makosa ya kigaidi, Amir Ibrahim, akasema hii ina maana kuwa mafundisho hayo ya dini yana viashiria vya ugaidi.

Amir Ibrahimu, akasema kama ni hivyo ni vyema Kamanda Siro, akatoa tafrisi sahihi ya ugaidi na gaidi ni nani, kwani mpaka sasa kuna Waislamu wapo magerezani baada ya Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwafungulia kesi za ugaidi na mpaka sasa hakuna ushahidi uliopatikana kwa zaidi ya miaka mitano sasa.

Akizungumzia suala hilo Sheikh Rajabu Katimba, alisema Waislamu wameingiwa na hofu zaidi baada ya kusikia kuwa ukaguzi huo wa Madrasa na Shule watashirikishwa timu ya kupambana na makosa ya kigaidi.

Alisema kwa anuani hii ya ugaidi, imeshaiathiri jamii ya Waislamu nchini kwani waliopo magerezani kwa tuhuma za ugaidi ni Walimu wa Madrasa, Masheikh, Walimu wa somo la Elimu ya Dini ya Kiislamu, viongozi wa Tasisis za Kiislamu na Waislamu wa kawaida.

Kauli hiyo ya Kamanda Siro, ya kufatilia mafundisho ya Dini imezua taharuki husasani kwa Waislamu, ambao kwa nyakati tofauti wamesema kuwa inaweza ikawaathiri zaidi wao kuliko watu wa dini zingine.

Kwa ujumla wamefafanua kuwa Jeshi la Polisi, mara nyingi limekuwa likitafsiri zaidi mafundisho ya Uislamu kuwa ni ugaidi na ndio sababu wengi waliokamatwa na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi ni Waislamu.

Akithibitisha hilo Imamu wa Masjid Salam Vingunguti, Sheikh Ibrahim Saidi, alisema wanakumbuka Polisi, walivyompiga risasi na kumuua Imamu Salumu na kudai alikuwa gaidi kwa kuwa alitamka ‘Allah, Akbar’ wakati anakufa.   

Kwa upande wake Ustadhi Yusuph Mlawa, alisema Madrasa nchini Tanzania, zimekuwa zikifundisha Dini tangu enzi na enzi na hazijawahi kuwa na matukio yeyote yanayosadikiwa kuwa ni ya kigaidi, katika historia ya nchi hii.

“Iweje hivi sasa hawa watu wa Jeshi la Polisi, waanze kutoa amri na maamuzi ya kipi sahihi kifundishwe na kipi kibaya kisifundishwe, hizi ndizo chokochoko.”

“Watakacho kitasababisha wawe tayari kukabiliana nacho, wanafanya yote haya kwa kutafuta radhi za wa-Magharibi na chuki zao binafsi dhidi ya haki, basi wajifunze tu historia ya dunia watatambua kwamba Uislamu na Waislamu ni watu wa amani.” Amesema Ustadhi Mlawa.

 

 

Latest News

Most Read

  • Week

  • Month

  • All