Seneta wa chama cha Democrats Marekani, amesema kuna uwezekano Rais Donald Trump kuwa gerezani kabla ya uchaguzi mkuu ujao nchini humo mwaka ujao 2020.

Seneta huyo wa upinzani, Elizabeth Warren ambaye ametangaza azma yake ya kugombea kiti cha rais katika uchaguzi ujao nchini humo, alisema hayo Jumapili iliyopita akiwa katika mkutano wa kampeni mjini Cedar Rapids, jimboni Iowa.

Huku akiashiria uchunguzi unaoendelea hivi sasa kuhusu uhusiano wa Marekani na Urusi, Seneta huyo amebainisha kile kinachotia wasiwasi ni kwamba, kufikia mwaka 2020, Trump sio tu hatakuwa Rais wa nchi, bali pia huenda asiwe mtu huru.

Mwanasiasa huyo wa Democrats alimtaja Rais Trump kuwa ni matokeo ya mfumo uliochakachuliwa na anayetumikia maslahi ya matajiri walio wachache na watu wenye ushawishi, huku akiwapaka matope watu wengine wote.

Rais Trump amekuwa akikosolewa na wapinzani na hata wapambe wake, wakiwemo wanachama wa chama tawala cha Republican.

Utafiti wa maoni uliofanywa na shirika la habari la CNBC hivi karibuni unaonesha kuwa Rais Trump, anaendelea kupoteza uungaji mkono sio tu miongoni mwa wananchi, bali pia miongoni mwa wafanyabiashara tajiri waliomuunga mkono katika kampeni zake za uchaguzi uliopita mwaka 2016.

Kwa mujibu wa utafiti huo, ni asilimia 34 tu ya mamilionea nchini Marekani ndio wameonesha kuwa watamuunga mkono Rais Trump katika uchaguzi ujao wa rais wa mwaka 2020, ikilinganishwa na asilimia 45 mwaka jana.Parstoday.