Bali njia salama za kutibu

*Vitamini D ‘dawa’ mujarab

Na Omar Msangi

 

Kufuatia vifo vilivyofuatana vikihusishwa na ugonjwa wa COVID-19, mitandao ya kijamii, imefurika taarifa na maoni mbalimbali juu ya ugonjwa huo.

Binafsi nimeguswa na ujumbe mmoja uliopata kushereheshwa katika moja ya vyombo vyetu vya habari, ukisema kwamba kutokana na vifo hivi, umefika wakati serikali iseme ukweli kwamba ugonjwa upo na kuchukua hatua.

Hoja nadhani sio, uwepo au kutokuwepo kwa ugonjwa wa COVID-19, lakini namna ya kukabiliana nao. Mheshimiwa Rais Magufuli anaposema kwamba jifukizeni, chukueni tahadhari, tumuombe Mungu, ni kukiri kwamba kuna tatizo.Nadhani ni muhimu kwanza tufahamu kwamba, janga hili limegubikwa na siasa na utata mwingi. Kwanza, ni juu ya chanzo chake. Inavyojuliana ni kwamba kirusi cha corona kipo, miaka nenda miaka rudi. Lakini je, hii Covid-19, ni ya asili (natural) au ya kutengeneza katika maabara?

Kama imetoka kwenye maabara, nani waliihandisi na kwa malengo gani? Je, kuingia mitaani na kuanza kuleta balaa, ilikuwa ni tukio la ajali au waliokihandisi kirusi hicho walikimwaga mtaani kwa makusudi? Nini lengo?

Taarifa za kuaminika za wataalamu mbalimbali, zinasema kwamba Covid-19 inatoka kwenye maabara. Ni corona iliyofanyiwa uhandisi.Tukikubali hilo, lazima kuibuke msururu wa maswali ambayo yanatutaka tuchukue tahadhari katika kupambana na janga hili ambalo ni wazi kwamba “limetengenezwa” na mwanadamu.Sasa inapotokea kwamba, wanaonyoshewa kidole kwamba ndio “wahandisi” wa Covid-19, ndio hao hao, wanaoibuka na ufumbuzi na kushinikiza kila mtu atumie “dawa” ama chanjo zao, hapo lazima maswali yazidi.Sura ya jambo hili inakuja katika mchezo wa ‘kuunda tatizo, unasambaza woga na kitisho cha tatizo hilo, kisha unakuja na ufumbuzi. Wanasema: “Kitisho au kuwafanya watu wahamanike kwa woga, ni makakati mzuri wa kuuza chochote unachotaka.”Ni katika mazingira haya, ndio maana muda wote Serikali imekuwa ikijitahidi kutoa miongozo ya namna ya kukabiliana na janga hili, lakini wakati huo huo, tusije kutumbukia katika mtego wa waliohandisi “Covid-19”, ambao sasa wanakuja na chanjo.Wakati napitia na kusikiliza taarifa kutoka mitandao ya kijamii, zilizokuwa zikichambuliwa na baadhi ya vyombo vya habari, ilinikumbusha makala moja niliyoisoma wiki iliyopita juu ya uwezo wa Vitamic D katika kukabiliana na Covid-19. Mwandishi wa makala hiyo anasema kwamba, Vitamini D imetajwa kuwa dawa mujarabu ya COVID-19.Hata hivyo, kinachowatatiza watafiti wengi, ni kwanini ukweli huo unafichwa na badala yake hupigiwa debe chanjo ambazo licha ya kuwa hazijafanyiwa utafiti wa kina, lakini ni ghali na zenye madhara.Makala inaeleza kwamba, ni katika mambo ya kushangaza kwamba wakati utafiti unaonyesha kwamba Vitamin D ina matokeo mazuri kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini wakiwa na COVID-19, na wakati ‘dawa’ hiyo, ni rahisi sana, karibu na bure, lakini huoni ikipewa kipaumbele.

Lakini baya zaidi ni kwamba, hata taarifa za tafiti juu ya umadhubuti wa tiba hiyo, huonekana kama zinafichwa kwa makusudi.Taarifa kama hizo zimeandikwa pia na gazeti la The Telegraph la tarehe 14 Februari, 2021. 

Katika habari hiyo, mwandishi Sarah Knapton ananukuu taarifa ya utafiti iliyofanywa na wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Barcelona wakisema kuwa Vitamin D imeonyesha uwezo mkubwa wa kukabiliana na Covid-19.

Katika uchambuzi uliopewa anuwani: “Why politicians and doctors keep ignoring the medical research on Vitamin D and Covid”, mwandishi Jonathan Cook, anasema kwamba, ni mwaka sasa toka tafiti mbalimbali zilipothibitisha umadhubuti wa Vitamin D katika kuzuiya maambukizi, halikadhalika kutibu Covid-19, lakini wanasiasa na madaktari wapigia debe chanjo, wameupa kisogo ukweli huo.

“Ni wakati wa kusema ukweli juu ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika tafiti zilizofanyika Hispania kwamba matumizi ya Vitamini D yamepunguza idadi ya watu wanaolazwa ICU na kuleta nafuu ya haraka kwa waliokuwa wamelazwa, lakini hawajafikia hatua ya kuwekwa ICU.” Anasema.

Hayo ndiyo yaliyosemwa pia na Dr. John Campbell akisema kwamba, tiba hiyo hupunguza vifo kwa zaidi ya asilimia 60.

Dr. Campbell na mwandishi Jonathan Cook, wameitaja repoti ya utafiti “Pre-Print Paper in the Lancet”, ambayo inaeleza kwamba idadi ya wagonjwa waliohitaji kuwekwa chumba maalum cha uangalizi wa karibu (Intensive Care Unit-ICU) katika wale waliolazwa kwa tatizo la Covid-19, ilipungua kwa asilimia 80 baada ya kubugia vidonge vya kuongeza Vitamin D.

Aidha, repoti ikasema kwamba ‘Dozi Kubwa ya Vitamini D’ (Large Doses of Vitamin D), ilipunguza vifo kwa asilimia 64.

Lakini kubwa zaidi, utafiti huo unaonyesha kwamba, dawa hiyo haina madhara kabisa (No Side-Effects) hata pale wagonjwa waliolazwa wanapopewa dozi kubwa (mega-doses).

“Hizi ni taarifa na takwimu zinazotokana na utafiti wa kisayansi ambazo zingepasa kuwa katika kurasa za mbele za vyombo vikubwa vya habari (lakini?), hasa katika kipindi hiki ambapo hakuna uhakika kwamba itapatikana “risasi moja tu ya maajabu inayoweza kuwa chanjo dhidi ya Corona.” Anasema mwandishi Jonathan Cook.

“Kama Vitamin D ni tiba kwa waliolazwa kwa matatizo ya Covid-19, ni wazi pia kwamba Vitamini hiyo itakuwa kinga mujarabu kwa ambao hawajaugua.” Aliongeza.

Kwa miaka mingi, tafiti zinaonyesha kwamba Vitamin D, ni tiba na kinga ya maradhi yanayoathiri upumuaji (respiratory infections), halikadhalika kutibu kile kinachoitwa kitaalamu: “chronic auto-immune diseases”, mfano wa kisukari, halikadhalika kuzuia mfuro wa seli. Kwa wanaojua Kiingereza mwandishi anasema:

“For many years, limited studies – ones that Big Pharma showed no interest in expanding – had indicated that Vitamin D was useful both in warding off respiratory infections and in treating a wide variety of chronic auto-immune diseases such as diabetes and multiple sclerosis by damping down inflammatory responses of the kind that often overwhelm hospitalised Covid patients.”

Hata hivyo, mwandishi huyo anasema kwamba tusishangae kuona wanasiasa na Makampuni Makubwa yanaipa mgongo Vitamin D kwa sababu, haina masilahi ya fedha.

Dunia imekuwa ni ya fedha. Vyakula vya Vitamin D au hata kama itakuwa ni kwa mfumo wa vidonge (Vitamin D Supplements) ni rahisi. Sasa makapuni ya kibeberu lazima yapige vita tiba hiyo.

Mwandishi anasema, hashangai kwa makampuni makubwa ya dawa kuchukua msimamo huo, lakini kinachoshangaza zaidi ni wanasiasa na wanasayansi!

Kwa nini wanapigia agenda ya watu walio tayari kuangamiza uhai wa binadamu ilimuradi wao wanapata pesa?  

Haya ni mambo ya ajabu kabisa, anasema mwandishi mmoja, akieleza kuwa wanasayansi, badala ya kushikamana na utaalamu, wanaburuzwa wanasiasa na wenye pesa na kuwataka watu wajifungie ndani, jambo linalopunguza masaa ya kupata jua na kufanya mazoezi ambayo ni muhimu kwa kujenga kinga ya mwili dhidi ya maradhi.

Katika kumalizia uchambuzi wake, Jonathan Cook, anasema kwamba, maadhali tafiti zimeonyesha kwamba Vitamin D ni dawa mujarabu ya Covid-19, jukumu la wananchi ni kuihimiza serikali kutoa fedha ili taasisi za utafiti ziongeze utafiti juu ya Vitamin hiyo, na kutoa elimu ya kuhimiza watu kula vyakula vyenye wingi wa Vitamin D, huku pia zikitengenezwa “Vitamin D Supplements”.

 

 

Most Read

  • Week

  • Month

  • All