Na Nizar K Visram, Dar es Salaam

HABARI kutoka makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) mjini Addid Ababa zinasema umoja huo unamuunga mkono Nicolas Maduro kama rais halali wa Venezuela. Haya yalisemwa na Thomas Kwesi Quartey, Naibu Mwenyekiti wa AU, baada ya kukutana na Modesto Leite, balozi wa Venezuela katika Umoja wa Afrika.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kwesi ametangaza uungaji mkono wa Umoja wa Afrika kwa raia na serikali ya Rais Maduro. Kabla ya hapo pia Jerry Matjila, balozi wa Afrika Kusini katika Umoja wa Mataifa alisisitiza kwamba nchi yake inamuunga mkono Rais Maduro na kwamba itaendelea na msimamo wake huo. 

Marekani, Canada, utawala wa Israel na baadhi ya nchi za Ulaya na eneo la Amerika ya Kusini, zimetangaza kumuunga mkono Juan Guaidó aliyejitangaza na kujiapisha kama rais wa Venezuela. Kwa upande wa pili nchi za Urusi, Iran, China, Uturuki, Mexico, Cuba, Afrika Kusini na nchi nyingine nyingi za dunia zimetangaza kumuunga mkono Rais Nicolás Maduro ambaye alichaguliwa mwaka jana na wananchi kuwa rais halali wa Venezuela.

Wakati huo huo nchi kadha duniani zimeilaani Marekani kwa njama zake chafu za kuingilia mambo ya ndani ya Venezuela, kuchochea fujo na machafuko nchini humo na kumtangaza Guaido kama rais. Juan Guaido, spika wa bunge aliyefutwa kazi, amejitangaza na kujiapisha kama rais bandia wa Venezuela. Siku iliyofuata Rais Trump akatangaza kumtambua.

Ieleweke kuwa kabla ya hapo Guaido alitembelea Washington na akiwa huko akapewa miongozo. Makamo wa rais wa Marekani, Mike Pence naye akamsihi Guaido kujitangaza akiahidi kumuunga mkono. Ndipo Guaido akajitangaza kama rais. Guaidó asili yake ni kada wa chama cha mrengo wa kulia, Voluntad Popular kinachofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) pamoja na shirika la National Endowment for Democracy (NED). Ni dhahiri kuwa yote haya yalipangwa kutoka Washington kama kawaida. Marekani imekuwa ikifanya haya katika maeneo ya Amerika Kusini (Latin America) kwa muda wa zaidi ya miaka mia moja.

Wakati haya yanafanyika, majeshi ya Venezuela yametangaza kumuunga mkono Rais Maduro na kuilaani Marekani kwa kuingilia mambo yao ya ndani. Na vyombo vya habari vya Magharibi vimecharuka kuonyesha wafuasi wa Guaido wakiandamana, wakati hatuonyeshi halaiki ya wananchi wanaomuunga mkono Maduro.

Mbinu hizi za Marekani nchini Venezuela zilianza tangu Rais Hugo Chavez aliposhika madaraka mwaka 1999. Venezuela ni nchi ya kwanza duniani kwa utajiri wa mafuta. Hayati Chavez akaamua kutumia utajiri huo kwa manufaa ya wavuja jasho. Akataifisha makampuni ya mafuta na kutumia mapato ili kuwapatia wananchi huduma za kijamii kama matibabu, elimu na makazi. Jambo hili liliwakwaza sana mabepari uchwara wa Venezuela na mabwana zao wa Marekani. Ndipo Wakaanza kuandaa mipango ya kumpindua Chavez.

Mwaka 2002 walifanikiwa kidogo kumuondoa Chaves, lakini mara moja wananchi walimiminika mitaani kote nchini wakitaka Chavez arudi haraka. Baada ya siku mbili tu vibaraka walilazimika kukimbia na kumuachia Chavez kiti chake. Ieleweke kuwa suala si demokrasia wala udikteta kama wanavyodai mabeberu. Chavez alichaguliwa katika uchaguzi ulioshuhudiwa na watazamaji wa kimataifa. Kati yao alikuwa rais mstaafu wa Marekani Bw Jimmy Carter, naye alisema hajaona dosari yoyote katika uchaguzi wa Chavez. Hata hivyo Marekani ikaiwekea Venezuela vikwazo vya kila aina ili kuiangusha kiuchumi.

Wakapiga marufuku Venezuela kuuza mafuta yake nchi za nje, wakanyakua fedha za Venezuela katika benki za kigeni, wakanyakua akiba yake ya dhahabu iliyo nchi za nje. Wakazuia Venezuela kununua au kuuza bidhaa nchi za nje. Alhasili wametangaza vita vya kiuchumi dhidi ya Venezuela. Halafu leo wanadai eti Chavez na mrithi wake Rais Maduro ni mafisadi walioshindwa kusimamia uchumi wa nchi!?

Ukweli ni kuwa mwaka 2005 uchumi wa Venezuela ulikua kwa asilimia 9.4. Hakuna nchi ya Amerika Kusini iliyofikia kiwango hicho. Mfumuko wa bei ulishuka. Kwa mujibu wa ripoti ya BBC, mwaka 2012 Venezuela iliongoza nchi za Amerika Kusini katika kupunguza umasikini na kuinua hali za wananchi. Hii ilisemwa hata katika ripoti ya CIA (factbook) ambayo iliungama kuwa Venezuela ilishinda hata Marekani katika kupunguza umasikini (Voigt, 2013). Haya ni matokeo ya sera za Chavez.

Lakini vikwazo haramu vya Marekani vikaongezwa. Ikawa vigumu kuuza mafuta katika soko la kimataifa. Venezuela ikakosa vipuli na bidhaa ghafi. Marekani ilitangaza vita vya kiuchumi dhidi ya wananchi wa Venezuela. Na vita vya kisilaha navyo haviko mbali, kwani Rais Trump na washauri wake, kina Pompeo na Bolton, wametamka wazi kuwa kuna uwezekano wa kuivamia kijeshi Venezuela. Ndio maana mnamo Septemba 2018 maafisa wa Marekani walifanya mkutano wa siri pamoja na baadhi ya wanajeshi vibaraka wa Venezuela. Wakala njama za kumpindua Maduro. Mara moja wananchi wakaingia mitaani na kuwalani vibaraka na mabwana zao.

Gazeti la The New York Times lilisema kuwa mazungumzo hayo ya siri yaliidhinishwa na Rais Trump. Hili si jambo geni kwa ubeberu wa Marekani. Mnamo Februari 2018 aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Bw Rex Tillerson alisema katika historia ya nchi za Amerika Kusini, makamanda wa jeshi huwa wanatumika kama vibaraka ili kuzipindua serikali zao.

Kwa mfano mwaka 1954 Marekani iliwatumia makamanda wa Guatemala ili kuipindua serikali ya Rais Jacobo Arbenz iliyokuwa imechaguliwa kidemokrasia. Badala yake wakawatawaza vibaraka wa kijeshi. Haya pia yalifanyika katika Brazil (1964), Bolivia (1964) na sasa wanajaribu kumpindua Rais Maduro.

Mnamo Agosti 2004 Marekani ilimteua William Brownfield kuwa balozi wake nchini Venezuela. Kwa mujibu wa mtandao wa Wikileaks kazi muhimu aliyokabidhiwa ni kutayarisha mpango wa kumpindua Chaves. Balozi huyo alitayarisha mpango huo na kuuwasilisha makao makuu Washington tarehe 9 Novemba 2006. Tarehe 27 May 2014 Wikileaks iliweka hadharani barua kutoka balozi wa Marekani nchini Colombia ikisema kuwa misaada yote imetayarishwa ili kufanikisha usaliti wa kumpindua Chaves. Barua hiyo ilieleza njia itakayotumika kupenyeza misaada hiyo hadi Venezuela. Misaada yenyewe ni pamoja na fedha. 

Njama kama hizi zimekuwa zikipangwa na Marekani tangu kufanikiwa kwa mapinduzi ya Venezuela 1999. Tangu wakati huo Marekani imekuwa ikimimina fedha kemkem ili kuyaangusha mapinduzi hayo kwa kuwahonga wasaliti.

Katika bajeti ya serikali ya Marekani kila mwaka fedha zimekuwa zikitengwa kwa ajili ya kuchochea fujo kwa kuwafadhili wasaliti wa mapinduzi. Wengi wao ni kutoka vyama vya upinzani pamoja na asasi za kiraia (NGO). Kwa mfano, katika bajeti ya mwaka 2014/15 Marekani ilitenga Dola milioni 5 kwa kazi hiyo na mwaka 2015/16 zilitengwa Dola milioni 5 na nusu. Ndipo mnamo Machi 2014 njama zilipangwa na wapinzani wenye siasa kali za mrengo wa kulia. Waliwaahidi wanajeshi vyeo na fedha, pamoja na visa za kuingia Marekani. Yaani Marekani iliwafagilia njia ya kukimbilia huko ikilazimika.

Februari 2015 njama zingine ziligunduliwa, lengo likiwa kuwahonga wanajeshi walio kazini na waliostaafu ili kuteketeza kwa mabomu miundo mbinu, ikiwemo jengo la bunge, mahakama kuu na vyombo vya habari. Haya yamekuwa wakiyafanywa na Marekani katika nchi za Amerika Kusini kama Guatemala, Brazil na Bolivia. Huko Chile mwaka 1973 waliangusha serikali ya Dakt. Salvador Allende iliyochaguliwa kwa kura halali na wazi, kwa sababu ya itikadi yake ya ujamaa. Walimuua Allende na badala yake wakampachika dikteta na muuaji Jenerali Pinochet.

Na kule Iran mwaka 1953 wakati alipochaguliwa kihalali Waziri Mkuu Mohammed Mosaddeqh, majasusi wa Marekani na Uingereza walimpindua. “Kosa” alilofanya ni kuamua kutaifisha visima vya mafuta ili mapato yake yatumike kwa maslahi ya wananchi. Mabeberu wakampachika mfalme kibaraka aliyeitwa Shah. Na hivi karibuni nchi kama Iraq, Libya, Afghanistan na Syria nazo zimeingiliwa kijeshi.

Visingizio wanavyotumia ni kuwa wanaeneza demokrasia duniani, eti wanawaokoa wananchi kutokana na watawala wa kidikteta. Huu ni unafiki, kwani kama wana nia ya kueneza demokrasia na utawala bora, basi wangeanza huko Marekani ambako serikali huchaguliwa kwa kura chache. Ni kawaida nchini Marekani kwa mgombea wa urais kuchaguliwa kwa kura chache na anayepata kura nyingi anashindwa. Ni pamoja na hila na udanganyifu katika upigaji kura.

Kuhusu Venezuela nia yao ilidhihirishwa na John Bolton, mshauri wa Trump alipotamka kuwa lengo lao katika kuipindua serikali ya Maduro ni kuyawezesha makampuni ya Marekani kudhibiti mafuta. Hii itaisaidia sana uchumi wa Marekani, alisema Bolton wakati akihojiwa na TV nchini Marekani.  

Na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Pompeo naye ametangaza kuwa serikali yake iko tayari kutoa Dola milioni 20 eti msaada wa kibinadamu kwa wananchi wa Venezuela wanaokabiliwa na upungufu wa chakula na madawa. Yaani Marekani iliyoiwekea vikwazo Venezuela tangu 1999 na kusababisha maisha magumu nchini humo, sasa eti wanatoa msaada wa kibinadamu. Wananchi wa Venezuela wanasema hii ni njama ya kuwahonga na kuwanunua ili waache kumuunga mkono Rais Maduro.

Ni vizuri ikaeleweka kuwa nchi moja kuivamia nchi nyingine au kula njama za kuangusha serikali yake au kuiwekea vikwazo, ni uhalifu wa sheria ya kimataifa. Kwa mujibu wa Mahakama ya Kimataifa (International Court of Justice) na kwa mujibu wa kanuni za Umoja wa Mataifa (UN), nchi moja kuiwekea vikwazo nchi nyingine ni kuingilia mambo yake ya ndani.

Hii imo katika sura ya pili, kifungu cha saba cha Mkataba wa UN (United Nations Charter) ambayo kila nchi mwanachama imesaini na kuridhia – pamoja na Marekani.

Halafu kuna Mkataba wa Umoja wa Nchi za Amerika (Charter of the Organization of American States). Sura ya 4 kifungu cha 19 cha mkataba huo kinasema hakuna nchi yenye haki au mamlaka ya kuingilia, kwa sababu yoyote ile, mambo ya ndani ya nchi nyingine.

Lakini kama tujuavyo, historia ya Marekani imejaa mifano ya uhalifu wa sheria ya kimataifa. Ni tabia ya ubeberu kutojali sheria na badala yake kulinda maslahi yake ya kibebebru. Uharamia huu unaonekana hivi sasa nchini Venezuela.  

(0658- 010308 This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.)