Colors: Orange Color

Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Ardern, ameahidi uwajibikaji wa serikali yake kuhusu ripoti ya hujuma dhidi Msikiti mjini Christchurch.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetahadharisha kuhusu njaa na hali mbaya inayowasumbua raia wa Yemen.

Akemea siasa “kongwe za Kisonge”

Borafya ataka makaburi yafukuliwe

Angalau ijulikane alivyoiba marehemu

 Na Mwandishi Wetu

Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi amekemea siasa za fitna, chuki, ubaguzi na utengano na kuhimiza umoja.

Katika kusisitiza hoja hiyo, akasema ndio maana ipo Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa mujibu wa Katiba ikiwa na lengo la kuimarisha amani, utulivu na kuwaunganisha wananchi ili kuhakikisha Zanzibar inakwenda mbele kimaendeleo.

“Watu wanasema Rais tumemchagua lakini kaiuza nchi kwa wapinzani, maana yake nini, maana yake ni kwamba wanasema mimi kufanya Serikali ya Umoja wa Kitaifa nimefanya kosa, ndugu zangu nataka kukwambieni katika nchi yoyote ukitaka kuleta maendeleo, lazima kwanza muwe wamoja wananchi wote ndio maendeleo yatapatikana.”

Amesema Mheshimiwa Rais Mwinyi na kuhoji “kwenye fujo, kwenye vurugu maendeleo yatapatikana vipi?”

Nasaha za Rais Mwinyi, bila kutaja kwa mifano hai, ni kujibu zile siasa za kale za Kisonge ambapo kila kukicha kulikuwa kukitolewa ujumbe wa kuonyesha Zanzibar imegawika katika makundi yanayo hasimiana ya walioshikilia Dola na wale wapinzani.

Dk. Mwinyi ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, alisema hayo wakati akizungumza na wananchi na wanachama wa CCM Mwa mjini Magharibi Unguja katika mkutano wa kuwashukuru wanachama kwa kukichaguwa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana.

Mwinyi amesema, Katiba ya Zanzibar ndio inayotaka kuwe na Serikali ya Umoja wa Kitaifa na sio yeye.

Dk. Mwinyi amesema bado Chama Cha Mapinduzi (CCM) kipo imara, bado wao wana Wawakilishi wengi kuliko chama chochote na pia wana wabunge wengi kuliko chama chochote ambapo chama chengine hawawezi kuwafanya chochote kwa sasabu wao wapo wengi na wanaweza kutekeleza wanachokitaka.

Aliwaambia wana CCM waache tabia ya kupiga majungu kwani hazitasaidia chochote katika maendeleo kwa kuwa uchaguzi umeshakwisha.

“Hizi fitina ziishe, kama kuna watu wamekasirika kwa nini nimepata mimi, ndio Mweyeenzi Mungu kishanipangia, Mweyeenzi Mungu ameshatwambia katika vitabu vyote kwamba Ufalme unatolewa na Mungu, kama uliyemtaka hakupata, basi rudi sasa tuwe wamoja yamekwisha yale,” alisisitiza Dk. Mwinyi.

Aliongeza kwamba anatambua fika kuwa ana mkataba na wananchi wa miaka mitano ambapo ana jukumu la kutekeleza kwa vitendo yale yote aliyoyaahidi wakati wa kipindi cha kampeni.

 “Nipeni basi nafasi nikamilishe ahadi zangu na pia mnipe nafasi kwa wale wanaotaka kunizuwia niwashughulikie kwa nguvu,” alisema Dk. Mwinyi huku akishangiriwa na kuimbiwa nyimbo ya ‘Mpewa hapokonyeki aliyepewa kapewa’.  

Dk. Mwinyi alisema hajaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa ajili ya kudhoofisha nguvu za CCM kama baadhi ya watu wanavyoeleza katika mitandao ya kijamii, bali lengo lake ni kuleta umoja mshikamano na maendeleo kwa wananchi wote.

Hata hivyo, kuonyesha namna Rais Mwinyi alivyofanikiwa kwa muda mfupi, mkongwe wa siasa za ‘Kisonge’, Mstaafu Mzee Borafya Silima amejitokeza hadharani na kusajili salamu zake za kuunga mkono hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Rais Mwinyi.

Mstaafu Borafya Silima ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini Magharibi, amemwomba Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar kuwachukulia hatua wahusika wa ubadhirifu wa fedha za umma.

Aidha amesema, ni vyema kufukuwa makaburi kuwatafuta watu waliohusika na ubadhirifu mkubwa wa fedha za serikali kama walivyotajwa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2019-2020.

“Umesema Bwana Mkubwa kuwa hutafukua makaburi, basi hata fedha za mazishi alizozikiwa huyu maiti hutaki kuzijua? Tukishazika tunarudi kunako jamvi, sanda shilingi 12,000, ubao, shilingi 5,000 marashi shilingi 1,000, gari iliyomchukua maiti kumpeleka Mwanakwerekwe shilingi 20,000, basi hata hizi hutaki kuzijua?”

Alihoji Borafya na kushangiriwa na kuungwa mkono kwa shangwe na vigelegele za wafuasi wa chama hicho.

Borafya alisema lazima ufike na hizi uzijue asifukuliwe maiti kwa kuwa kufukua maiti ni haramu, lakini fedha lazima zijulikane.

Awali katika hotuba yake Mheshimiwa Hussein Mwinyi alisema kwamba, yeye sio kiongozi wa kwanza kuunda muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, bali imeletwa na maridhiano ya kisiasa yalioafikiwa na kupelekea mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar. 

Aliwataka baadhi ya viongozi kuacha kuwachonganisha na wananchi katika suala hilo kwani faida za Serikali ya Umoja wa Kitaifa zimeanza kuonekana wazi wazi katika mshikamano wa wananchi katika kushiriki maendeleo.

Aliwataka baadhi ya viongozi kuacha ubinafsi wa kuona kwamba hawakufanikiwa kuingiza watu wao katika uchaguzi mkuu katika kinyanganyiro cha urais wa Zanzibar na ndiyo maana wameanzisha chokochoko hizo.

Mwezi wa Julai 30 mwaka 2010 Wazanzibari walipiga kura ya maoni kuamuwa mfumo gani wa kuendesha serikali wanaoutaka ambapo asilimia 66.4 walisema wanahitaji kuwepo kwa muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayovishirikisha vyama vya siasa ikiwemo wpainzani.  

Baada ya mazungumzo ya muda mrefu yaliofanywa na Kamati ya Maridhiano iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wake Mzee Hassan Nassor Moyo (CCM), Eddy Riamy (CCM) na Mansour Yussuf Himid (CCM) na kwa upande mwengine Abubakar Khamis Bakari (CUF) Salum Bimany (CUF) na Ismail Jussa (CUF), walifanya kazi kubwa ya vikao vya ndani katika kukubaliana suala hilo na mwisho kuafikiana. 

Hatimae Waasisi wa Maridhiano Malim Seif Sharif Hamad (CUF) na Dk. Amani Abeid Karume (CCM) wakati huo akiwa Rais wa Zanzibar walidhihirisha kwa umma na hatimae Novemba 2009 kupeana mikono Ikulu Zanzibar na kuwatangazia wananchi kuwa wamekubaliana kuondosha tofauti zao na kusahau yaliopita na kujenga Zanzibar mpya yenye siasa za kistaarabu na kuachana na yote yaliopita.

Mapema Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja kimesema kinaunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kupambana na ubadhirifu wa mali za umma na uhujumu wa uchumi.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi, Mohamed Rajab alisema wanaunga mkono juhudi zote zinazochukuliwa na Rais wa Zanzibar katika kupambana na uhujumu wa uchumi na matumizi mabaya ya fedha za serikali.

“Mheshimiwa Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi tunakuunga mkono juhudi unazozichukuwa katika kupambana na wabadhirifu na wafujaji wa fedha za serikali ambapo tunakuomba uendelee na mikakati hiyo hiyo”, alisema Rajab.

 

Latest News

Most Read

  • Week

  • Month

  • All