Na Bint Ally Ahmed

WANAFUNZI wa Darasa la Saba katika Shule za Msingi nchini, wanatazamiwa kufanya mtihani wao wa Taifa wa Elimu ya Dini ya Kiislamu Septemba 9 mwaka huu.

Katibu wa Islamic Education Panel (IEP), Mwalimu Shafii Hussein, akitoa taarifa juu ya mtihani huo amesema kuwa maandalizi yote muhimu juu ya mtihani huo yamekamilika na kwamba utafanyika kama ilivyotarajiwa.

Mwalimu Shafii amesema awali ilizoeleka mtihani huo wa Taifa kufanyika Agosti 8 kila mwaka, lakini mwaka huu imekuwa tofauti kutokana na janga la ugonjwa wa Corona, ambalo limesababisha maandalizi ya mtihani huo kuchelewa pamoja na kufungwa  shule kwa muda mrefu.

Alisema maandalizi ya mtihani huo mwaka huu yamechukua muda mfupi kutokana na walimu kufanya kazi kwa juhudi kubwa, kuhakikisha wanafunzi wanamaliza mitaala yao mapema na kujiandaa vyema na mitihani yao.

Hata hivyo mwalimu Shafii alisema ugonjwa wa Corona umesababisha baadhi ya shule kushindwa kujisajili kwa ajili ya kufanya mtihani huo kutokana na muda wa maandalizi kuwa hafifu.

Shafii ametoa shukran zake za dhati kwa Serikali hasa Ofisi za Elimu kuanzia Wilaya, Mikoa mpaka Taifa.

Aidha, amewashukuru pia wasimamizi na waratibu wa masomo ya Elimu ya Dini ya Kiislamu hapa nchini, kwa ushiriakiano wao wanaoutoa kwa Islamic Education Panel.

Ametoa wito kwa wazazi kuwahimiza watoto kuendelea kufanya maandalizi ya mtihani, hasa kwa kipindi hiki kilichobaki ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao.

Nao Wakuu wa Shule zote zilizojisajili kufanya mtihani huo, wameombwa kufuata taratibu na maelezo yote waliopewa ili kurahisisha zoezi hilo kufanyika sawia na kwa ufanisi.

Mwalimu Shafii amesema kuwa mwaka huu jumla ya shule 3,542 zimejisajili kufanya mtihani huo, huku idadi ya wanafunzi waotarajiwa kufanya mtihani huo wa Taifa ikiwa ni 124,732 nchi nzima.

 

 

 

 

Most Read

  • Week

  • Month

  • All