Tunawatakia kheri ya mwaka mpya Hijriya 1442

MWAKA mpya wa Kiislamu 1442 Hijria umeingia. Wakati tukifurahi kuingia mwaka huu, ni muhimu wale waliojaaliwa kuwa hai na afya njema, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwapa tunu hiyo adhim katika maisha.

Aidha, tunachukua fursa hii kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu magh’fira wale waliotangulia mbele ya haki na kuwaombea shufaa wale ambao ni wagonjwa, ili wapone na kurejea katika afya njema.

Wakati tukiwa tumeingia katika mwaka mpya wa Kiislamu, tumeona ni muhimu Waislamu na hata wasiokuwa Waislamu wakafahamu kwamba, kalenda ya Kiislamu iliasisiwa rasmi wakati wa Ukhalifa wa Omar Umar bin Khatab katika mwaka wa 16AH.

Ilikuwa ni baada ya mashauriano na makubaliano ya Masahaba (Ijmaa), hatimaye wakakubaliana tukio kubwa la ‘Hijra’ kuwa ndilo liwe nukta kianzio cha kuihesabu kalenda hiyo.

Tukumbushane tu kwa ufupi kwamba tukio tukufu la ‘Hijra’ lilichukuliwa kuwa mwanzo wa kalenda ya Kiislamu kwa kuwa ndilo lililoweka mpaka muhimu wa maisha ya Waislamu kuishi chini ya tawala ya kikafiri ndani ya Makka, na kuanza maisha mapya chini ya dola tukufu ya mwanzo ya Kiislamu ndani ya Madina.

Hijra ni tukio la safari aliyoifanya Mtume (S.A.W) kutoka Makka kuelekea Madina, ikiwa ni hatua muhimu katika harakati za kuutawalisha Uislamu kuwa mfumo wa maisha na kusimama Ukhalifah.

Mtume Muhammad (S.A.W) aliwasili Madina mwezi wa Rabil Awwal mwaka wa mwanzo Hijria. Akapokewa kwa vifijo, nderemo na hoi hoi, kwa kuwa alikuwa kiongozi aliyekuwa akisubiriwa kwa hamu. Baada ya kuwasili Madina, akaasisi dola ya mwanzo ya Kiislamu iliyodumu karne zote chini ya Makhalifa baada yake.

Wakati tukiwa katika mwaka huu mpya wa Kiislamu, ni muhimu tukakumbushana pia umuhimu wa Waislamu kujenga mazoea na kuiweka katika akili zao kalenda hii. Utamaduni huu utawawezesha kuweka mipango yao katika usahihi kwa mujibu wa Imani yao. Lakini pia kwa kufanya hivyo, kutaiwezesha jamii ya Kiislamu kuyaendea matukio muhimu ya kiimani na kutekeleza ibada zao kwa wakati sahihi.

Alhamdulilah, taratibu tunaona kalenda hii inaanza kuwakaa Waislamu kadiri muda unavyosonga mbele.

Hata hivyo, tunaona kwamba ni jambo muhimu kwa Jumuiya na Taaisi za Kiislamu nchini, zikaweka utaratibu mzuri wa kuadhimisha siku hii kwa vitendo, ili watu kuhamasika zaidi katika kuitukuza siku hii.

Kwa mfano, taasisi na Jumuia hizo zinaweza iwe ni kwa pamoja au kwa kila tawi, kuandaa tukio maalum la kuadhimisha mwaka mpya wa Kiislamu kama vile matamasha ya ujenzi wa vituo vya Kiislamu, kuzuru mahospitalini na kuwasaidia wagonjwa, kuanda hafla za kuwasaidia yatima, kuandaa harambee za kusaidia huduma za kijamii nk.

Lakini pia mwaka mpya wa Kiislamu uwe ni fursa kwa jamii ya Kiislamu kujitathmini, kujirekebisha, kupanga na kuweka malengo yao utekelezaji wa majukumu waliyojiwekea kwa kipindi cha mwaka mzima. Tufahamu kwamba kadiri miaka inavyosogea na umri nao hupungua. Hili ni somo tosha kwa Waislamu kusoma alama za nyakati na kuwa watu wasiosahau kujiandaa kwa ajili ya maisha ya Akhera.

Mwaka mpya wa Kiislamu utuzindue tukikumbuke kifo kinachotunyemelea kila uchao ili tukithirishe kufanya matendo mema na kuepuka yaliyo haramishwa.

Tumeingia Hijriya 1442, tudumishe upendo na kuvumiliana baina yetu ili umma wa Kiislamu uweze kusonga mbele.

Uislamu sifa yake ni upendo, uadilifu, amani, hekima, busara, kushirikiana, kujituma, kuvumiliana na kusamehe.

Ikiwa sifa hizi zitazingatiwa, hakuna shaka kwamba Waislamu watapiga hatua kubwa ya maendeleo na kuwa kiigizo chema katika taifa letu.

Tunawatakia kheri ya mwaka mpya Hijriya 1442.

 

Latest News

Most Read