Mwandishi wa Kitabu: Zanzibar na Kinyang’anyiro na Utumwa

Na Mohamed Said

SIWEZI kujidai kuwa nilifahamiana kwa karibu sana na Sheikh Issa bin Nasser Al-Ismaily, kwa kiwango nilichofahamiana na Sheikh Ali Muhsin Barwani na nduguye Sheikh Abdallah Muhsin. Nilikutana na Sheikh Issa bin Nasser Al – Ismaily, Muscat mwaka wa 1999, nyumbani kwa Sheikh Ali Muhsin.

Sheikh Issa bin Nasser, alikuja kunisalimu aliposikia kuwa niko Muscat na mimi ni mgeni wa Sheikh Ali Muhsin. Hii ndiyo siku tuliofahamiana.

Taarifa zangu zilikuwa zimenitangulia Dubai na Muscat baada ya jamaa waliokuwa kule baadhi yao kusoma kitabu cha Abdul Sykes, kitabu ambacho wengi walisema kuwa historia ile haiko mbali sana na historia ya yale yaliyotokea Zanzibar.

Kwa ajili hii basi Sheikh Issa Nasser, alikuwa kanisikia kabla hatujakutana. Nakumbuka katika mazungumzo yetu Ali Muhsin, alimuuliza Sheikh Issa Nasser, uandishi wa kitabu chake unakwendaje?

Kumbe wakati ule Sheikh Issa Nasser, alikuwa anaandika kitabu chake kilichokuja kuwa maarufu sana, ‘Zanzibar Kinyang’anyiro na Utumwa.’Kitabu hiki kilikuja kuongeza mengi katika kuelewa historia ya Zanzibar, ambayo kwa kipindi fulani toka mapinduzi yatokee ilionekana kama vile utafiti na uandishi wake umehodhiwa na wageni.

Sheikh Ali Muhsin Barwani, yeye tayari alikuwa keshatoa kitabu cha kumbukukumbu zake, ‘Conflict and Harmony in Zanzibar.’

Kabla ya kuja Muscat, nilikuwa nimekwenda Dubai, kiasi na nikaonana na Aman Thani, na kipindi kile alikuwa tayari kaandika kitabu chake maarufu, ‘Ukweli ni Huu.’

Kipindi hiki kilikuwa kipindi cha mwamko wa Wazanzibari, waliokuwa nje kuandika historia ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambayo kwa muda mrefu ilikuwa ikiandikwa na wageni ikiwa na upotoshaji mkubwa.

Huu ukawa ndiyo mwanzo wa wanafunzi wa historia ya Zanzibar, kuanza kusoma upande mwengine wa Historia ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Ilikuwa katika safari hii ya Muscat, ndipo nilipokuja kufahamiana na Dr. Harith Ghassany, msomi wa Harvard, ambae katika mazungumzo yetu akaniambia kuwa yuko katika kufanya utafiti kuandika kitabu cha historia ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Hakika kipindi hiki kilikuwa kipindi cha kuandika upya historia ya Mapinduzi ya Zanzibar. Mara kwa mara ninaposoma yanayoandikwa kuhusu Mapinduzi ya Zanzibar, kwa sababu ya yale niliyokuwa nayafahamu huwa nawakumbuka watu fulani maalum kwa sababu ya misiba iliyowakuta.

Mmoja katika hawa ni Sheikh Issa Nasser Ismaily., siku nilipokitia mkononi kitabu cha Sheikh Issa Nasser, nilisoma tabaruku ya kusikitisha, Sheikh Issa Nasser, alinyanyua kalamu na kuanza kitabu chake kwa maneno haya:

“Kwa ukumbusho wa marehemu Baba yangu Sheikh Nasser bin Issa Al-Ismaily na mashahidi wengine waliodhulumiwa roho zao katika mauwaji ya tarikh 12 Januari, 1964 huko Zanzibar.’’

Mara nyingi huwa nawatahadharisha ndugu zangu kwa kuwaambia kuwa wachunge sana ndimi zao na wachukue tahadhari katika maneno yao kwani historia ya Mapinduzi, imejaa mengi ambayo hapaswi mtu kufanya mzaha ila kunyanyua mikono na kuwaombea maghfira wale waliodhulumu na wale waliodhulumiwa.

Lakini wengi katika hawa kwa kutojua ukweli huwa wanafuata mkumbo wakiwa hawajui nini khasa kilitokea katika mapinduzi yale na baada ya mapinduzi.

Katika zindio la kitabu cha Sheikh Issa Nasser, aliloandika Prof. Ibrahim Noor Shariff, kuna neno kalitumia mara tano akilirudia, rudia akisema, ‘Nini kilichopatikana’ akifuatia na madhila nataabika kuyarejea tena hapa kwani si ya kuhadithia kwani kuyahadithia ni kurejesha upya machungu.

Historia hii ya watu kuuliwa pasi na sababu ni historia ambayo kwangu imekuwa kitu nikaja kukizoea kukisikia kila ninaposafiri nje ya Tanzania na kukutana na Wazanzibari tukakaa kitako kuzungumza.

Haitaki kufikiri sana mtu anajisikiaje kwa kufiwa na mzazi wake achilia mbali kwa mzazi wake kuuliwa na muaji ukawa unamjua. Baada ya mapinduzi Sheikh Issa Nasser, alifukuzwa kazi ikabidi aondoke Zanzibar aje Dar es Salaam, kutafuta maisha na akapanga moja katika nyumba za Abdul Sykes.

Siku moja katika mazungumzo alimuuliza Bwana Abdul, nini kilitokea kusababisha mauaji yale yaliyotokea Zanzibar.

Bila shaka Sheikh Issa, alimuuliza Abdul Sykes swali lile kwa kuwa alikuwa anajua ushawishi aliokuwanao katika siasa miaka ya 1950 wakati nchi zao Zanzibar na Tanganyika, zinatafuta uhuru wao kutoka kwa Waingereza na akikumbuka ule udugu uliokuwapo baina ya vijana wa Dar es Salaam na Zanzibar wa kutembeleana wakati wa ‘Sports’ na kualikana Zanzibar Club na kwengineko.

Jibu alilotoa Abdul Sykes, bila shaka lilimshtua Sheikh Issa Nasser. Dr. Harith Ghassany, ambae ndiye namnukuu hapa kutoka kitabu chake, ‘Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru’ anasema Abdul Sykes alimwambia Sheikh Issa Nasser, Bora tusiyazungumze mambo ya Zanzibar, kwa sababu tukiyazungumza urafiki wetu utavunjika.”

Mimi sikushangazwa na jibu lile kwani kwa kuwa nilikuwa pembeni kwa Dr. Ghassany, wakati wa utafiti wa kitabu chake nilijifunza mengi na niliyajua majuto ya hawa wazee wangu kwa yale waliyojitwisha.

Wazee wangu hawa wao walikuwa TANU kindaki ndaki waasisi na TANU na ASP ni ndugu, walitaka sana ASP ishike dola na walitoa msaada mkubwa kufanikisha Mapinduzi yale.

Kitu ambacho hawakukitegemea ni kuwa marafiki zao pia watakuwa wahanga wa mapinduzi yale na watapoteza maisha na kuacha vizuka na mayatima. Kifo cha Jaha Ubwa na Abdulaziz Twala ulikuwa ujumbe tosha kwao wao.

Mkasa wa Jaha Ubwa na Abdulaziz Twala nikiujua vyema hawa walikuwa katika ile duru ya marafiki wa baba yangu kutoka Zanzibar, ambayo huku Dar es Salaam, ilikuwa ikiunganika na vijana wengine maarufu mjini mfano wa Bwana Abdul Sykes.

Ilikuwa wakija rafiki wa baba yangu nyumbani baada ya vifo vya Jaha na Twala baba alikuwa hawezi kuyataja majina yao kwa sauti, atanong’ona anapouliza hali za wake zao na watoto.

Namkumbuka rafiki ya baba yangu akiitwa Yunus huyu alikuwa akija nyumbani mara nyingi sana na alikuwa Afisa wa Polisi Zanzibar. Nilikuwa nikisikiliza mazungumzo yao wakati tuko mezani tunakula.

Baba alikuwa akishusha sauti na Baba Mzee Yunus na yeye alishusha yake pia wanapozungumza kuhusu hali iliyokuwapo Zanzibar. Kuuliwa kwa baba yake Sheikh Issa Nasser, hili kwa kila namna utakavyo litazama, hili lilikuwa zito sana.

Sheikh Issa Nasser, alipokamilisha kuandika kitabu chake akawasiliana na mimi na akaniletea vitabu Dar es Salaam, nivitawanye Zanzibar na Bara. Kwa bahati mbaya sana kitabu hiki kiliingia nchini mwaka wa 2000 na ikasadifu kulikuwa na uchaguzi Mkuu. Nilipokea makaratasi kuwa mzigo wangu umewasili bandari ya Dar es Salaam, nikauchukue.

Haraka sana nikamkabidhi ‘clearing agent’ makaratasi akautoe mzigo wangu. Nilishangaa nilipoambiwa kuwa mzigo wa vitabu, ‘Zanzibar Kinyang’anyiro na Utumwa’ kweli umewasili Container Terminal Dar es Salaam, lakini hauonekani popote pale.

Sheikh Issa Nasser, alikuwa akiniletea ‘email’ kila siku kuniuliza kuhusu vitabu na jibu siku zote lilikuwa lilelile kuwa vitabu havionekani.

Kumbe vitabu vilikuwapo lakini vimezuiliwa kwa kuogopa Uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka wa 2000, uliokuwa jirani unakaribia. Wataalamu walikisoma kitabu na wakaona wakati haukuwa muafaka kwa kitabu hiki kusomwa Zanzibar na kukipiga marufuku dhahiri halitakuwa jambo la busara kwani kitawapa Wazanzibari hamu zaidi ya kukitafuta.

Kwao wakaona jambo lenye nafuu ni kukizuia hadi uchaguzi ukisha watakiruhusu kutolewa bandarini. Baada ya uchaguzi kitabu kiliachiwa kikatoka na kiliuzwa kwa haraka sana Zanzibar na Bara.

Mwaka wa 2015, Nilirudi Muscat na nilikuwa na hamu sana ya kuonana na Sheikh Issa Nasser, lakini nilifahamishwa kuwa ni mgonjwa sana kwa hiyo sikuweza kumuona.

Allah amfanyie wepesi katika safari yake na wafiwa awape subra.

Amin.

Most Read

  • Week

  • Month

  • All