Neema Maumba Islamic Foundation yakaribisha  Ramadhani.

Na Bint Ally Ahmed

Neema Maumba Islamic Foundation

yakaribisha  Ramadhani.

Na Bint Ally Ahmed

Taasisi ya Neema Maumba Islamic Foundation yenye Makao Makuu yake Buguruni Jijini Dar es Salaam, imefanya hadhara ya kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kuwakumbuka wazee waliofanya kazi kubwa ya kuupigania Uislamu katika uhai wao na sasa wametangulia mbele ya haki.

Hadhara hiyo imefanyika katika viwanja vya Madrasat Neema Maumba, vilivyopo Ilala Jijini Dar es Salaam March 19.

Akizungumza kwenye hadhara hiyo, Sharif Habibu Hussein Badawi kutoka Malindi Kenya, ambaye ni mtoto wa Al-Marhumu Hussein Badawi, alimpongeza Ukht. Neema Maumba kwa jitihada zake za kuenzi kazi kubwa iliyofanywa na baba yake mzazi, Mzee Alhaj Yusufu Maumba na kutoa wosia kwa waliohudhuria hadhara hiyo kujitahidi kufanya shughuli kama hizi katika majumba yao.

“Nikupongeze kwa jambo hili, kuzungumzia wazee namna walivyokuwa wakijitoa kuhakikisha dini yao inasonga mbele kwa kutumia mali na muda wao mwingi kwa jambo hili, nashukuru Mzee Maumba, alikuwa ni kiigizo chema, aliifanya kazi ya dini kwa moyo wake wote, sehemu yake imekwisha, tuliobaki tuna kazi ya kuendeleza shughuli hizi, tuhakikishe hatutoki katika njia ya haki,” alisema Sharif Badawi.

Alisema Al-Marhumu Mzee Maumba, alijitahidi kuacha  sadaka zenye kuendelea, kama vile madrasa na sasa inaendelea kusomesha watoto wa Kiislamu dini yao.

“Nakumbuka aliwahi kutoa kiwanja kule Morogoro na kinaendelezwa, ni vizuri na sisi  tukaiga tabia hizi njema kwa Al-marhumu Mzee Maumba, kwa hichi alichokiacha kwani jambo jema linapendeza kuigwa, ili nasi tukapambana kuendeleza harakati na tutakuwa tunakumbukwa kwa mazuri yetu,” aliongeza Sharifu.

Kwa upande wake Neema Maumba, ameahidi kuendeleza harakati zilizoasisiwa na baba yake mzazi, ikiwamo kusomesha dini vijana wengi kwa kadri Allah atakavyomjalia na harakati zote alizoziacha marehemu baba yao.

“Hili jambo la kuukaribisha mwezi Mtukufu wa Ramadhani lilikuwa likifanyika toka enzi za uhai wa baba yetu, ilikuwa kila kabla ya wiki mbili kufikia Ramadhani, Mzee Maumba alikuwa anafanya hauli ya kuukaribisha Mwezi mtukufu, na sisi wanawe tunaendea kufanya hivyo” alibainisha Ukht. Neema.

Alisema wao waliiga tabia hizi za kuukaribisha mwezi Mtukutu kutoka kwa baba  na mama yao, ambao walikuwa wakifanya jambo hilo kwa muda mrefu katika umri wao na kwamba, nao hawana budi kuiga tabia hizo njema kutoka kwa wazazi wao hao, Mungu awa rehemu huko waliko.

Neema Maumba ambaye pia ni Mratibu wa Udugu Social Help Welfare, yenye Makao Makuu yake Buguruni Jijini Dar es Salaam alisema anajisikia faraja kuona jambo hilo linafanyika kwani ni jambo lenye kheri mbele za Allah.

Maumba, ambaye amepata bahati ya kuratibu Kundi la Udugu lenye wanachama zaidi ya 20, alisema jambo hilo litakuwa endelevu kwa uwezo wa Allah.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Sharifu Mageta, alisema amefurahi kusikia kutoka kwa Sharifu juu ya umuhimu wa kufanya hauli majumbani, kwani ni jambo jema na lina tija.

“Nimesikia hapa kutoka kwa kiongozi kuwa si dhambi kuwataja waliotangulia, kuzungumza mazuri yao na kuyatakafari jinsi ya kuyaenzi, nadhani ni nukta muhimu ya kuchukua,” alisema.

Hadhara hiyo ambayo ilihudhuliwa na watu  mbalimbali akiwemo mama maarufu mwanaharakati Bi. Aisha Sururu, Mwenyekiti wa Wanawake  Bakwata Taifa Bi. Mariamu Mtambo na Bi. Mariamu Dedesi, Mwanaharakati maarufu hapa nchini.

Mbali na watu hao, pia hadhara hiyo ilihudhuliwa na madrasa mbalimbali  za eneo la Buguruni.

 

 

Latest News

Most Read