Na Hamis Mataka

SHULE ya Msingi Mchikichini sikupata kushika zaidi ya nafasi tatu za juu muda wote wa miaka saba hapo shuleni. Kwa kuwa nilianza darasa la kwanza nikiwa na umri wa miaka 11, ule moja wa miaka minne ambayo ningekuwa shule ya msingi iliniwezesha kumiliki Chuo changu mwenyewe yaani Madrasa, nikiwa Mwalimu Mkuu, katika umri mdogo wa miaka 15.

Nilipoanza Shule darasa la kwanza katika umri huo wa miaka 11, ambao ni mkubwa kwa kuanza darasa la kwanza, pale Shule ya Mchikichini nilikuwa pia mwalimu wa dini kwa wenzangu.

Kwa ajili ya makuzi yangu ya Kiislamu, nilikuwa nikitoka eneo la Shule tu nilivaa Kanzu yangu juu ya sare kwa kuwa sikujisikia kuvaa kaptula mitaani, kwani uchi wa mwanaume unaanza juu ya magoti yake.

Mwalimu wangu wa Historia Mzee Kasunsumo alipata kuniambia:

“Sheikh Khamis, pamoja na uwezo wako wa kielimu hutochaguliwa kwenda Sekondari na kinachokuponza ni huu Ualimu wako wa Dini ya Kiislamu.”

Hakika na kweli ikawa hivyo, badala ya kuchaguliwa kwenda sekondari nikapelekwa Chuo Cha Ufundi Chang'ombe kusomea Usukaji Mota. Uhodari wangu wa masomo na tabia yangu nzuri hazikutazamwa. Kilichoangaliwa ni ule Uislamu wangu.

Sikukaa sana pale Chuo Cha Ufundi na kwa hakika moyo wangu ulikuwa ukiniuma nikiwaona wale ambao mimi nikiwapita katika masomo wako sekondari wanasoma na mimi nimepelekwa Chuo Cha Ufundi nikiwa muhitimu wa darasa la saba. Kilichofuatia ni kuwa nikaacha katikati na kujiunga na Chuo Cha Biashara ambapo nilichukua Basic Book-Keeping Certificate (BBC) na kufanya vizuri sana.

Katika mitihani ya ndani, “I was first out of 67 candidates,’’ yaani nilikuwa mwanafunzi wa kwanza nikiongoza katika wanafunzi 67. Huu ndiyo ulikuwa uwezo wangu mimi mwanafunzi niliyotokea Shule ya msingi Mchikichini na Maalim wa Madrasa mtoto.

Nilipokabidhiwa cheti cha BBC taarifa ya ufaulu ilinizuia kuendelea na NABOCE kwa ibara hii: “If you are Standard Seven you will be eligible to sit for NABOCE Exams after you have completed formal Form Four Education.’’ Bahati mbaya ilikuwa inazidi kuniandama.

Wakati huo umasikini wa familia ulinilazimisha kufanya kazi za kutafuta riziki halali mbali ya kuendelea kufundisha dini katika Chuo changu. Baba yangu Sheikh Saidi Mnuta Mataka, akinilazimisha kuoa mapema ili amuone mjukuu wa jina lake kabla hajafa.

Nilioa.

Sasa kwa ajili ya kizingiti kile cha kuwa na cheti cha kidato cha nne, nililazimika kuitafuta elimu ya Sekondari kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (National Correspondence Institute) na nikafaulu QT (NECTA) Mtihani wa Kidato cha Nne na nikaweza kurudi chuoni CBE kuendelea na masomo ya NABOCE huku nikipata ajira ya kudumu ya Mfasiri wa Lugha za Kiarabu, Kiingereza na Kiswahili katika moja ya Balozi nchini.

Laahawla! Chuoni sikuikuta tena NABOCE bali mtaala mpya wa ATEC I na II nami nikazisoma kozi husika nikafaulu na nikaweka cheti kibindoni. Lakini ajira mpya ya Ubalozi haikuendana na mambo ya uhasibu nikalazimika kubadili upepo na nikasoma Lugha ya Kiingereza na kufanikiwa kutunukiwa Diploma ya Lugha (Kiingereza).

Muhimu leo nikuandikiapo haya nimeweza kupata vyeti hivi vifuatavyo hapo chini:

  1. B.A. (Philosophy, Religious Studies & Kiswahili) - OUT.
  2. Post Graduate Diploma (Education) - UDSM.
  3. M.A. (Education) - UDSM.
  4. Post Graduate Diploma (Management) - IGNOU/UDSM under Pan African E-Network (African Union/Government of India) through Tele-Conference facility.
  5. Post Graduate Diploma (Human Resource Management)- IGNOU/UDSM.

Hapa nilipo sasa In Shaa Allah nasubiri MBA (HRM) baada ya kuwasilisha tasnifu yangu juu ya Time Management kupitia utafiti nilioufanya IFM, Dar es Salaam chini ya Dr. Adam Jamal kwa anuani hii:

“Managing Time Effectively: A Case of Lecturers in the Higher Learning Institutions.’’

Sasa hivi ni mwanafunzi wa LLB anayefikiria kuja kufanya Comparative Study kati ya Islamic Law na Conventional Law (Common Law and Others).

Kinachofurahisha siku ya Graduation wale waliounga unga elimu na waliounganisha husimama mstari mmoja kutuzwa.

 

   

Latest News

Most Read