Na Bakari Mwakangwale

SHEIKH Amran Kilemile amehoji Umma wa Kiislamu umefanywaje mpaka umekuwa hivi katika hali ya kuzorota katika mambo mbalimbali ya kijamii na kushindwa kuwa kitu kimoja.

Sheikh Kilemile amehoji hayo katika Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, uliofanyika Jumamosi ya Januari 5, 2019, katika ukumbi wa City Gurden, Gerezani Jijini Dar es Salaam.

Mbele ya Waislamu waliohudhiria Mkutano huo Mkuu wa mwaka, Sheikh Kilemile alionyesha kuguswa na kusikitishwa kwa kuzorota kwa Umma wa Kiislamu katika juhudi za kimaendeleo husan kumiliki ardhi na kuzitumia kwa maendeleo yao.

“Ndugu zangu tumefanywaje sisi, nauliza Umma huu umefanywaje mpaka umekuwa hivi, yanafanywa mambo na wenzetu mbele yetu, sisi tupotupo tu miaka inakwenda, hatuna umoja, hatuna agenda.”

“Sasa yaliyopita si ndwele, tugange yajayo lililo muhimu ni kuungana na kuungana sio Sunna ni Faradhi, umoja huo ulenge kukabiliana na hali tuliyo nayo sasa (tusonge mbele).” Amesema Sheikh Kilemile.

Akawataka Waislamu kutozipa nafasi tofauti zao ndogondogo na kupelekea kukwamisha mipango na maendeleo yao.

Akaeleza kuwa Waislamu wamekatazwa kufarakiana ila wanaweza kutofautiana kimawazo na kifikra na kwamba kutofautiana si haramu katika Uislamu.

“Kufarakiana ndiko hakutakiwi, bali kutofautiana kupo, hakuepukiki lakini pia kutofautiana huko kuwe ni kwa kulenga maendeleo ikiwa wewe utafanya mwingine aje afanye tofauti zaidi ya awali na hiyo inakuwa ni tofauti ya kheri.” Amesema Sheikh Kilemile.

Alisema, ili kupiga hatua hivi sasa, Umma wa Kiislamu ufikirie zaidi kujenga umoja na mshikamano.

Akasema, katika kuharakisha maendeleo kwa Waislamu kupitia Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, ipo haja ya kuorodhesha matatizo ya Waislamu kila mahali kisha Waislamu wenyewe washirikishwe namna ya kuyakabili.

Alisema, kwa ujumla Umma wa Kiislamu una matatizo mengi na hawawezi kuyatatu nje ya umoja wa kweli.

Aliyataja matatizo hayo kuwa ni elimu, uchumi na kubwa zaidi ni kule kukosa umoja.

Sheikh Kilemile, alisema ni jambo la msingi kujenga ushirikiano baina ya Baraza Kuu (viongozi) na Mabaraza mengine ili kuleta picha ya pamoja kwa nia ya kujenga umoja na mshikamano.