Na Mohammed Said

ALLAH ana njia za ajabu sana katika kuwatengenezea waja wake mambo yao. Nakumbuka kama ilikuwa jana vile siku moja miaka ya mwanzoni 1970.

. Nilikuwa naumwa na ilipofika jioni, nikawa nimezidiwa sana lau kama asubuhi nilikwenda hospitali na kupata matibabu. Mama yangu aliponitazama na kuona sina nafuu na hali inazidi kuwa mbaya, akawa anawaambia ndugu zangu:

“Huyu hebu apelekwe kwa Mwalimu Ramadhani Abbas akamuombee dua homa gani hizi zisizokwisha?’’

Nyumba yetu ilikuwa jirani ya kituo cha taxi cha Mkwajuni Mtaa wa Sekenke Kinondoni. Akatumwa mtu amwite dereva wa taxi jina lake Daudi Kingaru, rafiki yangu na mwalimu wangu wa dini akinisomesha hili na lile kila tulipokuwa pamoja, iwe nimemkodi au tumekaa chini ya mkwaju katika kituo cha taxi akisubiri abiria. Daudi Kingaru alikuwa mwanafunzi wa madrasa ya Shariff Abdulrahman, moja ya madrasa kubwa Dar es Salaam. Daudi alipofika mama akamuuliza:

“Daudi sahib yako kakamatika leo nina hofu isije kuwa ni upepo. Hivi Mwalimu Ramadhani Abbas yuko wapi siku hizi?”

Nikamsikia kwa mbali Daudi Kingaru anajibu, ‘’Chuo kimehama huku Mkunguni chini kipo Mkunguni juu kupita kwa Chaurembo.’’ Mimi homa imenishika kweli kweli nimevaa bukta na imelowa kiasi kiunoni kwa jasho kwani usiku kucha sikuweza kupata usingizi kwa joto la mwili. Kwa ufupi nilikuwa mahututi na nilipochukuliwa kupelekwa kwa Mwalimu Ramadhani Abbas, taarifa zilizoenea kwa marafiki zangu walipokuja kunijulia hali ni kuwa nilikuwa mahututi nimepelekwa hospitali. Tumefika kwa Sheikh Ramadhani Abbas inakimbilia Magharibi na nina hakika wazee wale walikuwa hawajaonana miaka mingi. Uhuru ulikuja na changamoto nyingi kuna baadhi ya nyumba Mtaa wa New Street sasa (Lumumba Avenue) zilikuwa zimevunjwa na nadhani hii ni pamoja na nyumba kilipokuwa chuo cha Mwalimu Ramadhani Abbas kilichokuwa Mkunguni na New Street na hivyo kuhamia hapa kilipo hivi sasa. Waliovunjiwa nyumba mtaa ule walipewa na serikali nyumba nyingine Mwananyamala. Huu ni wakati wa Shirika la Nyumba la Taifa kuondoa nyumba mbovu na kujenga makazi mazuri kwa wananchi wake.

Mwalimu Ramadhani Abbas alikuwa mbali ya kusomesha watoto dini alikuwa pia ni tabibu. Hakuna mtoto atakaezaliwa Kariakoo katika miaka ile ya 1950 tuliyozaliwa sisi na asipelekwe kwa Mwalimu Ramadhani. Wengi tumepita katika mikono yake kwa kuombewa dua na mengineyo. Hii ndiyo iliyomfanya mama amkumbuke Mwalimu Ramadhani Abbas na aamue nipelekwe kwake baada ya mimi kuumwa.

Nakumbuka ulikuwa Mwezi wa Shaaban na Mwalimu Ramadhani Abbas alikuwa amefunga siku hiyo. Mama akamueleza shida yangu na mengine ya ziada kutaka dua za kutuliza ubongo wangu utulie nimjue Allah na nishikamane na sala. Hivi ndivyo walivyokuwa wazee wetu. Sheikh Abbas Ramadhani Abaas huyu Mudir wa sasa Madrasa Abbasiyya alikuwa chini ya miguu ya baba yake anatambaa. Iko siku nilimweleza haya kwa hakika alipigwa na butwaa kubwa. Nikamwambia, ‘’Abbas mimi nimekujua wewe ukiwa mchanga pale kwenu.’’

Sheikh Ramadhani Abbas akamwita Sheikh Zubeir wakati ule ana umri kama wa miaka 15 au 16 hivi, akamwambia anichuke twende kwenye madrasa akanifanyie kisomo.

Hivi ndivyo nilivyokuja kufahamiana na Sheikh Zubeir Yahya. Tulipendana kuanzia siku ile na nilifurahi sana nilivyomuona alivyokuwa akisoma nikamuomba anifundishe na mimi Qur’an na akanipangia siku za kwenda kwa ajili ya kisomo na kusoma. Mama akawa ananishajiisha nisikose kwenda hadi dua ikamilike. Katika kipindi hiki cha mimi kwenda pale Madrassa Abbasiyya, ndipo nikamuomba Sheikh Zubeir anisomeshe Qur’an vizuri na yeye akakubali akanianzisha alif kwa kijiti. Ilikuwa si kazi ndogo kumtoa William Shakespeare kichwani kwangu niliyomezeshwa na mwalimu wangu wa Lugha ya Kiingereza Miss Menez na kufuta mashairi maarufu ya Kiingereza mfano wa ‘’The Ancient Mariner,’’ na kuingiza Qur’an kichwani kwangu. Ikawa Sheikh anashirikiana na Sheikh Pongwe (sasa ni marehemu) kijana mwenzake kunisomesha na kwa hakika walinifanya mwanafunzi maalum. Nilikuwa naanza darasa kwa Sheikh Zubeir kunisikiliza aliyonisomesha siku iliyopita kisha naendelea. Hiki kilikuwa kipindi muhimu sana katika maisha yangu.

Alhamdulilah Sheikh Zubeir akanipa alichonipa na Allah atamlipa kwa hisani hii aliyonifanyia mimi. Nami sikuacha kila siku kuwaeleza watu kila nilipokutana na Sheikh kuwa ni mwalimu wangu na yeye alikuwa hasemi chochote ila kutabasamu. Sheikh Zubeir akawa sasa si mwalimu wangu tu, bali ni pia rafiki yangu wa karibu sana.

Kipindi hiki msikiti wa Mtoro Mwinyi Mangara ule mdogo, umevunjwa na umejengwa msikiti mpya chini ya uongozi wa Sheikh Abdallah Chaurembo na Sheikh Kassim Juma. Msikiti huu ulipendwa sana na kulikuwa na darsa maarufu la tafsir ya Qur’an akisomesha Sheikh Abdallah Chaurembo mwanafunzi mkubwa wa Sheikh Hassan bin Ameir. Sijapatapo kumsikia mwanazuoni anayesomesha tafsiri ya Qur’an kama alivyokuwa anasomeshsa Sheikh Abdallah Chaurembo. Unatamani jua lisimame uendelee kumsikiliza na kumsikiliza. Alipatapo kunambia mwalimu wangu mwingine Sheikh Ali Abbas kuwa: ‘’Usisikitike kuwa hukupata kuhudhuria darsa la Sheikh Hassan bin Ameir anavyosomesha tafsiri ya Qur’an. Hivyo anavyosomesha Sheikh Chaurembo ni kama alivyokuwa akisomesha mwenyewe Sheikh Hassan, kuanzia namna yake hadi sauti. Sheikh Abdallah kamuiga mwalimu wake kila kitu hakuacha chochote.’’

Sheikh Zubeir akawa kanianzisha safari yangu ya kutafuta ilm lau kwa uchache. Nikawa sasa siogopi tena kupokea juzuu kwenye khitma. Nikitoka Abbasiyya sasa natia mguu Msikiti wa Mtoro ikawa sikosi darsa la Sheikh Abdallah Chaurembo na katika waliokuwa wanahudhuria darsa hii alikuwa mwanafunzi mwengine wa Sheikh Hassan bin Ameir, Sheikh Ramadhani Abbas, mwalimu wa mwalimu wangu Sheikh Zubeir na Sheikh Digila. Sheikh Zubeir akiniona niko nimekaa namkabili Sheikh Chaurembo nasikiliza tafsiri ya Qur’an, alikuwa akifurahi sana. Hii darsa ni kama naiona vile. Masheikh wengi na maimamu wa misikiti mingi walikuwa wakija kusoma pale. Sheikh Kassim Juma alikuwapo, Sheikh Digila, Mzee Bofu, Mzee Mazongera, Maalim Mzinga, Mzee Mavemba, Mohamed Khan kuwataja wachache. Hawa walikuwa na nafasi zao maalum wakipenda kukaa wengi wao kwa utu uzima wakiwa wameegemea ukuta na nguzo za ndani za msikiti. Kulikuwa pia na kundi kubwa la vijana wadogo wa umri wangu na wakubwa zetu kidogo katika darsa hii.

Sheikh Zubeir akawa kanifundisha njia nyepesi ya kusomesha Qur’an hasa kwa watoto wa ndugu zetu ambao mazingira yamekuwa magumu sana kwao, mtindo wa maisha yao umekuwa hatarishi kwao na kwa watoto wao bila ya wao wenyewe kutambua hatari hii. Nikaamua kuwa na madrasa nyumbani kwa wanangu na watoto wa jirani na kwa miaka mingi tukawa na madrasa nyumbani Msasani Peninsula kwa watoto wa maofisa wenzangu na walimu walikuwa Ma Shaa Allah hodari wakaweza kufanya watoto waipende Qur’an.

Katika madrasa hii akahitimu mtoto wa kwanza wa kike akiwa na umri wa miaka 13. Huyu bint kwa ajili ya kuwa na msingi mzuri wa Qur’an akawa anaongoza shuleni kwake katika lugha ya Kiingereza. Nilikuwa hata mimi nikimsikia akizungumza Kiingereza ninasikia raha. Alikwenda baadae Kenya kuendelea na elimu ya sekondari akawa pia huko anaongoza kiasi akawa ndiyo msomaji wa matangazo yote kwa lugha ya Kiingereza katika, ‘’School Assembly.’’ Mwanafunzi huyu na yeye taarifa zikafika kuwa hata huko shuleni akawa anawafunza wanafunzi wenzake kusoma Qur’an. Wanafunzi wote wa madrasa hii (sasa ni wakubwa wameoa na kuolewa) wakawa wanafunzi wazuri hadi vyuo vikuu ndani na nje ya nchi. Elimu ya Sheikh Zubeir ikawa imeenea na kufika mbali sana. Naamini sheikh amefariki yeye mwenyewe hajui ni ushawishi gani aliacha kwetu.

Madrasa ya Abbasiyya haikuterereka baada ya kifo cha Sheikh Ramadhani Abbas badala yake madrasa ikazidi kung’ara. Sheikh Zubeir na Sheikh Abbas Ramadhani Abbas wakachukua uongozi wa madrasa kwa mafanikio makubwa. Maulid ya Mfungo Sita ya Abbasiyya hakuna asiyeyajua. Zafa yake huanza kwa fat’ha nyumbani kwa mama yetu Bi. Bahia aliyekuwa mke wa Sheikh Mzee Comorian mmoja katika wanafunzi wa Sheikh Hassan bin Ameir. Zafa ya Abassiyya inasimamisha mji kwa muda kuyapisha na usiku wake ndiyo yanasomwa Maulid uwanja umejaa pomoni.

Mwezi uliopita siku moja nikapokea simu kutoka kwa mtu ambae simfahamu kwa sura lakini tunawasiliana katika mtandao akanipa taarifa kuwa Sheikh Zubeir kampa maagizo anipigie simu anifahamishe kuwa ananiita na niende kwake na Balozi Dau. Huyu ndugu yangu akanifahamisha kuwa sheikh ni mgonjwa na yuko Kigamboni. Ikasadifu kuwa Balozi alikuwa amekuja Dar es Salaam, basi nikampigia simu na kumpa salamu za Sheikh Zubeir. Tukaenda kumwona Sheikh Zubeir asubuhi moja siku ya Jumapili. Tulimkuta Sheikh akiwa katika hali nzuri ya uchangamfu na ya kutia matumaini.

Tulizungumza na kuchekeshana sana tukikumbushana mambo mengi ya zamani. Fikra yangu ilikuwa sasa Sheikh afya yake inaimarika na atanyanyukia In Shaa Allah na tutakuwa pamoja Msikiti wa Mtoro ambako yeye ndiye alikuwa Imam Mkuu.

Maziko ya Sheikh Zubeir yameingia katika historia ya maziko makubwa sana yaliyopata kushuhudiwa Dar es Salaam. Hapakuwa na nafasi ndani ya msikiti hata ya kujibanza. Nje ya msikiti watu walikuwa wamejazana sehemu ya kina mama ndani ya msikiti ni hivyo hivyo. Jeneza lake lilipotoka naelezwa kuwa lilivamiwa na umma na mwendo wake ulikuwa wa taratibu mno kwa jinsi watu walivyokuwa wengi jeneza likitanguliwa na bendera na dhikr.

Silsila ya Sheikh Zubeir imewagusa wanazuoni wakubwa wengine kawaona kwa macho yake mwenyewe akiwa mwanafunzi hapo Abbasiyya alipoanza kusoma mwaka wa 1962 akiwa na umri wa miaka saba. Uongozi wake Abbasiyya na Mtoro uliziunganisha taasisi hizi na watu wake kuleta umoja na nguvu kubwa katika jamii ya Waislamu wa Dar es Salaam. Kuwako kwake katika taasisi hizi kuliwavuta wengi kuwa karibu na shughuli za maendeleo ya Uislamu.

Tunamwomba Allah alikunjue kaburi la Sheikh Zubeir alijaze Nuru na amtie Peponi.