Na Ben Rijal

Ramadhani ipo milangoni. Tumemaliza mwezi wa Rajabu na sasa tupo mwezi wa Shaaban kabla ya kuingia Ramadhan, mwezi ambao Muislamu aliokuwa balighi mwenye akili timamu, sio mgonjwa afunge.

 

Anajitia udarweshi ikifika Ramadhani, anavaa nikabu ikifika Ramadhani, husali ikifika Ramadhani, ikimalizika Ramadhani anaendelea na ufirauni wake. Anavaa nguo za heshima ndani ya mwezi wa Ramadhani tu.

Anasali sala za tarawehe katika mwezi wa Ramadhani tu na anashika jamaa madhubuti ndani ya mwezi wa Ramadhani, unaopomalizika haonekani tena.

Kauli za kawaida kuwasikia maimamu mbalimbali na kutoa tamko. Sala za tarawehe hujaa watu kwenye kumi la mwanzo na ifikapo kumi la pili hupungua mpaka ikabakia safu mmoja. Wenye kusali Ramadhani mpaka Ramadhani wana mashaka.

Kwa kweli kauli hizi sio kauli zinazotakikana kutolewa, bali sisi kama waumini tukiwaona wenye kuvaa nikabu ndani ya mwezi wa Ramadhani, tufurahi na tuwashajiishe huwenda akaselea kuivaa nikabu katika miezi mengine.

Wengine hushindwa kuingia misikitini kwakuchelea kunangwa. Maimamu wanatakiwa wajawe na furaha pale anapouwona msikiti wake umejaa maamuma na awe anatoa mawaidha ya kuwatia moyo wenye kuingia msikitini Ramadhani hadi Ramadhani.

Ramadhani nayo inataka mataarisho yawe ya vyakula, na hata mavazi. Mwingine hupendelea akenda kusali awe amevaa kanzu na kofia. Wengine hupenda kuziweka sadaka zake katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani na wengine hujitahidi kujitaarisha kuwasaidia mayatima.

Matayarisho kwa mwezi wa Ramadhani ni muhimu, na zaidi iwe katika kujitayarisha vipi utatekeleza ibada. Inahitajia muumini awe na mpango uliotimia wa kufanya matayarisho katika kufanya ibada. Kwa kutekeleza hayo nafsi yako utaiona inakupa heko, kwani utajikuta mwenye furaha, utajikuta maingiliano yako na wenzako katika kutenda mambo ya kheri yanaongezeka.

Hebu angalia maandalizi yangu kwa kifupi tu, mtu ambaye ni mvivu wa kutopea. Naandaa mpango wangu mzima wa mwezi wa Ramadhani pasi na kutaka kuuona umepanguka. Nitaianza siku kwa kuamka saa 9 za usiku nile daku baada ya daku sitolala ila nihakikishe kwanza nimesoma Juzuu mmoja ya Qur’an. Kisha nitahakikisha na Sali sala ya alfajiri sala ya jamaa na kuhakikisha sitosali nje ya safu ya mbele. Baada ya sala nitakaa kitako kimoja na kusoma juzuu nyengine kisha kurudi nyumbani kujitayarisha na kwenda kazini. Nitapokuwa kazini nitajiepusha kadri niwezavyo kusema maneno ya ovyo na kujiweka mbali na upigaji wa soga. Nitapokuwa nimekaa kimya, nitahakikisha namsalia Mtume SAW alau kwa siku najiwekea taratibu ya kumsalia mara alfu.

Nitahakikisha nitapokuwa nipo njiani kurudi kazini, nitajiweka mbali na vishawishi vya kila aina na walenitawakosea kwa njia ya aina yoyote ile nitamwambia ‘’mie nimefunga.’’

Alasiri nitahakikisha sikosi darsa itakayokuwa inasomeshwa Qur’an na nitarudi nyumbani baada ya kusali sala ya Magaharibi. Nikishapata kufuturi, nitakaa kwa namna ya mapumziko bila ya kulala, kuangalia televisheni, kusoma gazeti kama namna ya kuisubiri adhana ya Isha. Baada ya adhana nitajitahidi kuwa wa mwanzo katika watakaofika msikitini tayari kwa kusali sala ya Isha na kusali tarawehe pamoja na witri. Ikifika saa 5 nitakuwa kitandani nimeshalala nikisubiri kula daku saa 9 za usiku.

Nitajaribu kulizungusha gurdumu hili kwa kila siku na ikifika kumi la mwanzo  limemalizika, nitajitathmini nimeweza kutimiza mpango niliojipangia. Nikiona sawa nitafarajika, nikiona niko nje na mpango mzima, nitaanza kujitilia mashaka na kuangalia vipi nijirekebishe. 

Kwenye kumi la pili nitazidisha kasi na nitahikisha kukaa itikafu ndani ya kumi la mwisho.

Bila ya kujipangia, ukawa unajiendea tu, mtu hutoweza kujitathmini. Wazee wetu waliopita walikuwa na mipango madhubuti kuliko haya nilioyanukuu. Mkulima anafika kutolima kwa mwezi mzima na kusema amejipanga kwa kufanya ibada. Mwaka mzima anaweka akiba ya chakula na ya fedha ili Ramadhani iwe yeye na msikiti, msikiti na yeye, mvuvi hivyo hivyo na wengineo, waliamini huo sio mwezi wa kulala wala wa kuufanyia mchezo kwa kujitahidi kujiweka karibu kwa kutenda ibada. Wakisema ndio tunatakiwa tufanye kazi ila wao hio wakisema ni kutenda ibada kwa kasi kubwa.

Jee, kwenye matumizi najipangaje au utajipangaje? Mtafiti mmoja wa nchi ya jirani katika utafiti alioufanya wa kuhojiana na watu 40, amekuja kuona kuwa asilimia zaidi ya 80 ya watumiao simu za mkononi kila siku husema uwongo sio chini ya mara 5 hadi 10. Kwa kweli simu za mkononi au wengine hupenda kuzita za viganjani, wenye kuzitumia husema uwongo wa kila aina, hudanganya, hufanya ulaghai wa kila sura na huzitumia katika kufanya machafu kama kuangalia picha zisofaa na kuzisambaza. Maradhi haya ni makubwa na kuweza kuepukana nayo. Fursa kubwa ni mwezi wa Ramadhani unaotukabili.

Nitachofanya lengo langu ni kukata matumizi ya simu kwa zaidi ya asilimia 50. Jambo la kwanza nitajiondoa kwenye makundi (magurupu) kwa asilimia 70. Sitoiangalia mitandao ya jamii zaidi ya mara mmoja kwa siku, nitatumia zaidi SMS za kawaida, nitapokuwa msikitini alasiri, nitazima kabisa simu mpaka nitapokwenda kufuturu. Sitoipa simu nafasi ya kunituma ila mie nitaituma simu nitakavyo mie. Ifikapo tarehe mosi Ramadhani nitaweka vocha ya shilling alfu tano ambayo nitataka niende nayo hadi kuingia mfungo mosi. Naamini nitaweza na nikiweza somo hilo, ndio nitakwenda nalo katika miezi iliobakia.

Nitajilazimisha kila kwenye majalisi ya kheri iwe sikosekani. Nitajitahidi kuhudhuria mashindano yote ya kuhifadhisha Qur’an sio tu nitahudhuria, ila nitakuwa mhudumu, nitashirikiana na waandaaji wanitume kwa kadri wawezavyo kutokana na ujuzi mdogo nilio nao.

Kubwa ambalo ndani ya mwezi wa Ramadhani mja analotakiwa kulitafuta ni ‘taqwa’, yaani kumcha Allah. ‘Enyi mlioamini! Mmeandikiwa kufunga kama walivyoandikiwa waliokuwa kabla yenu, ili mpate kuwa na takua’’ (Baqara 2: 183)

Neno taq’wa ni kumcha Allah na utapojielekeza kwa muumba na kujitolea nafsi yako kutenda mema na kufwata yale yote aliyokuja nayo Mtume Muhammad SAW. Utapoweza kufanya hayo, utajikuta umejengeka kiroho na unapojengeka kiroho huwa unatakasika.

Tathmini? Leo katika maendeleo ya ulimwengu tunaoishi kuna kujitathmini na huku ni katika kuweza kujiendeleza na kuweza kufikia mafanikio. Nitatoa mfano wa mja mwema aliowahi kuishi katika karne iliopita. Ilikuwa kila siku baada ya sala ya isha akimuuliza mwanawe na kumwambia sema kweli ninayokuuliza Allah anakuona, akawa anamuuliza:

 ‘’Jee, kutoka asubuhi hadi saa hizi umeshasema uwongo mara ngapi?’’

Kijana naye pasi na kutetereka humwambia mara 6 siku ya pili akamuuliza tena akajibu mara 4 ikenda hivyo hivyo hadi kufikia kijana inampitikia siku nzima hajaweza kusema lolote lile lilokuwa la uwongo.

Sasa mimi na wewe tuanze kuzijenga nafsi zetu na kuzitakasa tuone vipi tunaweza kujengeka kiroho.

Imam Ghazali anaeleza nafsi katika moyo huwa sawa na kisahani au kioo kilichokua hakina doa. Pale unapoanza kufanya dhambi, huingia kidoto na kidoto hicho kila unapoendelea kufanya dhambi, hutapakaa mpaka kukaingia kiza, hauonekani weupe na unapofika katika hali hio, huwa haingii nuru ndipo pale Waswahili wanaposema:

 ‘’Hasikii la muadhini wala muasha taa msikitini.’’

Mtu anapofanya makosa anatakiwa atubie dhambi zake zifutike na tunapofanya baya tunatakiwa tufwatishe na jema ili lile baya lifutike.

Tunaishi na watu ambao hutenda mema nusu na kugubikwa na baadhi ya maasi kwa kudhani kishafanya ibada ya sala imetosha. Ukiona mtu wa namna hio, ujue kuwa ni katika wale ambao moyo umeshachafuka.

Tukae na tutafakari namna ambayo Ramadhani itapoingia tuwe watu wengine kabisa na hilo ukiliweza wewe mmoja kubadilika nyumbani kwako asaa na mke naye atabadilika na watoto wakafwata.

Ikiwa katika nyumba mmoja kuna watu watatu, falsafa hii wameiweza kwenye mtaa wa watu alfu mmoja tukasema kwa wastani watu 2 kwa kila nyumba ni kusema watu alfu mbili. Chuo cha Ramadhani kimeweza kuwajenga kiroho. Tukiendelea hivyo hivyo kwenye shehia au kata, utakuta mwisho ndani ya wilaya mmoja mwezi wa Ramadhani imewajenga kikweli waumini tuseme alfu ishirini, tukifika kwenye ngazi ya wilaya watazidi mara dufu na tukifika mkoa kuelekea ngazi ya taifa idadi itakuwa kubwa matokeo yake mpaka taifa litafika kuwa na nidhamu kutokna na ‘’Spirit’’ ya Ramadhani walivyoifahamu Waislamu.

Tusiifanye Ramadhani iwe ya kula na kuvimbiwa. Tusiifanye Ramadhani ni ya kucheza bao, keram, karata wahed wa sitin, kuangalia video 4 kwa siku. Tuifanye Ramadhani kutekeleza ibada na kujitakasa.

Niseme mie na wewe uitikie kuwa tunaisubiri Ramadhani kwa hamu. Ishabisha hodi mie ninaisubiri na nitajitahidi kadri niwezavyo nibadilike na wewe iwe hivyo hivyo.