Shule ya Kiislamu Kaloleni, Moshi yateketea kwa moto

Na Bint Ally Ahmed

Mabweni ya Shule ya Kiislamu ya Wasichana Kaloleni iliyopo Moshi yameteketea kwa moto wakati wanafunzi hao wakiwa katika bwalo la chakula, wakipata kifungua kinywa kabla ya kuingia madarasani.

Akiongea na An-nuur, Kamanda  wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Emanuel Lukula, amethibitisha kutokea tukio hilo shuleni hapo asubuhi ya tarehe  26, Agosti na kwamba, moto huo umeteketeza  mabweni ya wasichana shuleni hapo.

Hata hivyo alisema, chanzo cha moto huo bado hakijabainika na kwamba uchunguzi bado unaendelea kufanyika na ukikamilika watatoa taarifa kamili.

Awali akitoa taarifa ya kutokea ajali ya moto huo, Sheikh Mbwana Urari, Mjumbe wa Bodi ya wadhamini taasisi ya Direct Aid Society, alisema kuwa moto umeteketeza kila kitu katika mabweni hayo ya wanafunzi wa kike.

Amesema, walichobakiwa nacho wasichana wa shule hiyo ni nguo walizokuwa wamevaa tu.

Sheikh Urari alisema kuwa pamoja na uharibifu mkubwa uliotokea  kwa kuungua mabweni na vifaa vyote vya wanafunzi,  wanashukuru Mungu kwa kuwa hakuna mtu aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa, si  wanafunzi wala wafanyakazi.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii shuleni hapo Ustadhi Yahaya Jeremia, amesema kuwa wakati tukio hilo linatokea, wanafunzi wote walikuwa bwaloni kwa ajili ya chakula, hivyo hawakuweza kuelewa moto huo ulisababishwa na nini.

Aidha, miundo mbinu ya shule hiyo ilikuwa iko vizuri haikuwa chakavu kiasi cha kutiliwa shaka kusababisha moto huo.

Hata hivyo Bw. Jeremia amewatoa hofu wazazi na walezi kutulia na kuzidi kuwaombea dua  watoto wao wapate utulivu wa nafsi na moyo, huku wakiamini kila kinachotokea Allah ndio mtoaji.

“Tuendelee kusubiri taarifa kutoka vyombo vya usalama, wao watatupa taarifa juu ya chanzo au sababu ya kadhia hii”. Alisema Bw. Jeremia.

Sheikh Jeremia ametoa shukrani za dhati kwa niaba ya shule na uongozi wa Direct Aid Society, kwa serikali nzima ya mkoa wa Kilimanjaro, Jeshi la Zimamoto kwa namna walivyofanya juhudi katika kukabiliana na janga hilo.

Aidha, amewashukuru wote walioshiriki katika kadhia hiyo, hasa wanafunzi, walimu na wafanyakazi pamoja na majirani wanaozunguka shule hiyo na wale  wote walio wasaidia kuhakikisha moto huo wanaudhibiti bila kuleta madhara makubwa zaidi shuleni hapo.