Mlemavu wa macho ashinda mashindano ya Qur`an kina mama

Na Bint Ally Ahmed

Bi. Sikitu Juma Mohamed (40), mke na mama wa watoto wawili mwenye ulemavu wa macho kutoka mkoani Tabora, amekuwa mshindi  maalum katika mashindano ya kina mama ya kuhifadhi Qur`an yalioandaliwa na taasisi ya Ummul Muuminina Aisha Foundation (UMAIF) na kufanyika katika ukumbi wa City Garden, Kariakoo jijiji Dar es Saalam hivi karibuni.

“Kiu na mapenzi yangu ya kushiriki mashindano ya Qur`an ilikuwa ni kubwa, sijawahi kukata taama kutokana na ulemavu wangu wa macho, kwa mara ya kwanza nimeshiriki mashindano ya Qur’an yaliyoandaliwa na UMAIF na nimeweza kuibuka mshindi”. Amesema Bi. Sikitu Juma Mohamed wakati akiongea na mwandishi wa gazeti hili.

Amesema kuwa alipopata nafasi ya kuingia kwenye mashindano hayo ya wanawake, alijisikia furaha isiyo kifani kwani aliona kuwa anakwenda kutimiza ndoto yake ya miaka mingi ya kukutana na kushindana na wanawake wenzake.

Aliongeza kuwa matamanio yake sasa ni kuona wanawake wengi wa Kiislamu wakihamasika kusoma na kuhifadhi maneno matukufu ya Qur’an katika vifua vyao, kwani mwanamke akiijua vyema kuitumia Qur’an katika maisha yake, hakika atafanikiwa kuilea familia yake.

Aidha Bi. Sikitu amewataka wanawake wa Kiislamu walio na ulemavu kuona kuwa hakuna sababu ya kukaa nyumbani kwasababu ya ulemavu walionao alimradi wana afya.

Bali watoke majumbani mwao waitafute elimu popote ilipo ili wamjue Mola wao.

Bi. Sikitu pia ametoa wito kwa wale waliojaaliwa uwezo na Allah kujenga Madrasa (vyuo) maalumu kwa walemavu, ili waweze kuisoma dini yao.

Alisema, zitakapojengwa madrasa zinazozingatia mahitaji maalumu kwa kuwa watakaokuwa wanasoma hapo ni watu maalumu, Waislamu wengi wenye ulamavu watavutiwa kuisoma dini na kuleta manufaa makubwa katika jamii, tofauti na sasa ambapo wanakutana na changamoto kubwa, hasa miundombinu rafiki na kukosa watu wa kuwapeleka madrasa.

 “Nimekuwa napata shida sana pale ninapotaka kwenda Madrasa, sikuwa na mtu wa kunishika mkono, muda mwingine nashindwa kabisa kwenda madrasa kwasababu ya kukosa mtu wa kunifikisha na kunichukua madrasa, hii ni changamoto kubwa  ninayokutana nayo” Alisema Bi. Sikitu.

Aidha Bi. Sikitu aliwapongeza na kuwashukuru walioanzisha mashindano hayo kwa kina mama watu wazima, kwani wanawake wamekuwa wakishughulishwa zaidi na mambo mengi majumbani mwao hasa ya ulezi wa watoto na familia kwa ujumla.

Pamoja na kukabiliwa na majukumu hayo ya kifamilia, alisema ni vyema wakajihimu kutenga muda wa kuisoma Qur’an kwa kuwa huo ndio muongozo wa maisha yanayompendeza Mwenyezi Mungu.

Bi. sikitu amehoji, kama yeye ni mlemavu na analazimikiwa na kuitafuta elimu ya muongozo wa Allah, je ambae ana uwezo wake wa viungo timamu na hana tatizo lolote kimaumbile,  atamueleza nini Mwenyezi Mungu siku ya Kiama kwa kutoijua Qur`an pale maisha yake yatakapokatika hapa duniani?

Bi. Sikitu Mohammed ni mke na mama wa watoto wawili aliyezaliwa katika kitongoji cha Mwinyi, Tabora mjini. 

Alizaliwa bila ulemavu wa macho, alikuwa mzima na kuolewa hali ya kuwa anaona, lakini ghafla alipoteza neema hiyo ya kuona akiwa tayari amekwishaolewa na kupata mtoto moja.

Baada ya kupata mtoto wake wa kwanza, alianza kuhisi tofauti katika uwezo wake wa kuona, nuru ya macho ilianza kufifia, alianza kuona ukungu na baadae  akaanza kuona giza na hatimaye kutoona kabisa.

Alihangaika hospitalini huku na kule kutafuta tiba ya macho yake lakini hakufanikiwa na baadae macho yalizima kabisa.

Bi. Sikitu anasema kuwa katika kuhangaika kwake  kutafuta matibabu ya kurudisha uwezo wake wa kuona, alifanikiwa  kufika  Hospitali moja jijini Mwanza, ambapo alipelekwa na dada yake.

Alifanikiwa kuonana na daktari wa macho na baada ya kumfanya vipimo, ilionekana mishipa ya macho yake imekufa kabisa na hiyo ikawa ndio sababu kubwa iliyosababisha yeye kutokuona.

Baada ya kupewa taarifa na mtaalamu ambaye ni daktari bingwa wa macho, kwamba mishipa ya macho yake imekufa kabisa na hana uwezo wakuona tena, alimshukuru Mwenyezi Mungu.

“Hakika hii ni kadari ya Allah, mimi sina cha kusema mbele ya maamuzi yake Yeye aliyenipa macho haya, kaamua alichonikadiria”, alishukuru Bi. Sikitu.

Safari ya Bi. Sikitu kusoma kitabu cha Allah (Qur`an) ilianza miaka minne iliyopita, ambapo katika muda huo, amefanikiwa kuhifadhi Juzuu mbili.

Anasema kuwa njia anazotumia kuhifadhi Qur’an hali ya kuwa haoni, ni mwalimu wake wa Madrasa Ust. Issa Haji Iyoyota, ambaye anamtajishia aya za Qur`an na baadae yeye anamfuatilia kama vile anamwimbisha kidogo kidogo hadi aya hiyo inakaa akilini, na baadae  anaendelea na aya inayofuata. Hiyo ndio njia anayotumia kuhifadhi Qur`an.

Aidha Bi. Sikitu anasema kuwa njia nyingine anayoitumia kuhifadhi Qur`an akiwa nje na madrasa, ni kusikiliza kupitia simu au Redio.

Muda mwingi anapokuwa nyumbani akijishughulisha na kazi zake za nyumbani husikiliza Qur’an hadi aya zile zinakaa kichwani. Anapofika Madrasa mwalimu anamsikiliza namna alivyohifadhi aya hizo.

Bi. Sikitu amesema kuwa alishawishika  kusoma na kuhifadhi Qur`an  baada ya kusikiliza mawaidha kutoka kwa Sheikh mmoja kupitia Redio moja hapa nchini.

Sheikh huyo alikuwa anaelezea umuhimu wa kusoma Qur`an na alitoa kisa kimoja cha Swahaba katika enzi za Mtume (s.a.w), ambaye alikuwa ni mlemavu wa macho lakini alifanikiwa kuhifadhi Qur`an.

Ndipo Bi. Sikitu alipoona naye anayo nafasi ya kufanya hivyo, kwani hana udhuru wa kumfanya asihifadhi kitabu hicho cha Allah (SW), kama Swahaba huyo aliweza, naye ataweza kufanya hivyo kwa idhini ya Allah.

Bi. Sikitu anasoma katika Madrasa ya kina mama ya Markaz, iliyopo Mwinyi Tabora. Anasoma masomo ya Hadithi, Fiqh na Tauhid.

Hali ya Bi. Sikitu kimaisha sio nzuri kwa kuwa mume wake hana kazi ya uhakika na kipato chake sio cha uhakika, ‘anabangaiza’ tu.

Hata hivyo Bi. Sikitu anajishughulisha na kilimo cha mahindi na kuyauza  kwa rejareja na kusaidiana na mumewe katika kulipa ada za watoto.

Kama umeguswa na simulizi hii na unatamani kumsaidia Bi. Sikitu chochote ulichojaaliwa, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba yake 0785 588 747.

 

 

Latest News

Most Read

  • Week

  • Month

  • All