Kwa miaka mingi kumekuwepo na dhana na upotoshaji mwingi kuhusu nafasi ya mwanamke na hadhi yake katika Uislamu.

Wengi wakipotosha na kuaminisha watu kwamba Uislamu ni Imani inayomkandamiza mwanamke na kumuondolea thamani yake, huku wakiaminisha umma kwamba utamaduni wa Kimagharibi ndio ulioleta demokrasia ya kijinsia.

Sasa ni vyema tukajibu swali iwapo Uislamu unamtazama mwanamke kuwa ni sawa na mwanaume kama binadamu au unamuona ni wa hadhi ya chini kuliko mwanaume. Kuhusiana na haki za mwanaume na mwanamke, Uislamu una falsafa yake maalum ambayo ni tofauti, yale yaliyotokea miaka 1400 iliyopita na yanayotokea hivi sasa.

Uislamu hauamini kuwa katika mambo yote mwanaume na mwanamke wana haki na majukumu yanayofanana. Katika mambo fulani haki na majukumu yao ni tofauti na matokeo yake ni kuwa katika baadhi ya mambo nafasi yao inafanana na ya wanaume na katika baadhi ya mambo haifanani na ya wanaume.

Hii sio kwa sababu Uislamu, kama falsafa nyingine, unamtazama mwanamke kwa dharau au jinsia yake sio bora kama ya mwanaume. Uislamu unazitofautisha jinsia hizi mbili kwa sababu nyinginezo za msingi.

Unaweza kuwasikia wafuasi wa mifumo ya Kimagharibi wakitaja kanuni za Kiislamu kama vile mahari, matunzo, talaka, ndoa za mitala na mengineyo, kuwa haya yote ni kama matusi kwa mwanamke na yanashusha hadhi yake. Wanawapotosha watu kuwa sheria na kanuni hizi hazina maana na ulazima na zinamfanya mwanaume kuonekana ni bwana mkubwa.

Wanasema kwamba katika kipindi chote cha historia, kabla ya karne ya 20, sheria na kanuni zote duniani ziliwekwa kwa kuzingatia kuwa mwanaume ni mwenye jinsia bora zaidi na kwamba, mwanamke aliumbwa kwa maslahi na starehe ya mwanaume. Sheria zilizopitishwa na Uislamu pia ziko hivyo hivyo, zinampendelea mwanaume.

 

Wanadai kuwa Uislamu ni dini ya jinsia ya kiume. Hawamtambui mwanamke kuwa ni binadamu kamili na wanadai hii ndio sababu haujampa haki sawa na mwanaume. Kwamba ungekuwa unamtambua kuwa ni binadamu kamili, usingeruhusu ndoa za mitala (mke zaidi ya mmoja), usingehesabu ushahidi wa wanawake wawili kuwa ni sawa na wa mwanaume mmoja, usingeamuru gawio la mwanamke liwe nusu ya gawio la mwanaume, usingeamrisha papangwe bei ya mwanamke chini ya kivuli cha mahari na usingemfanya mwanamke awe tegemezi kwa mwanaume kwa upande wa matunzo, badala ya kufanya ajitegemee kiuchumi na kijamii.

Wanasema kuwa kwa kuzingatia yote haya, ni dhahiri kuwa mafundisho ya Uislamu yanamtazama mwanamke kwa jicho la dharau. Kwamba Uislamu unadai kuwa dini ya usawa lakini katika mahusiano ya kifamilia hakuna usawa wowote uliozingatiwa.

Wao wanashikilia kuwa katika suala la haki, Uislamu unampendelea waziwazi mwanaume na ndio maana umempa miliki zote hizi.

Tukipenda tunaweza kuweka hoja yao katika muundo wa kimantiki kwamba, kama Uislamu unamhesabu mwanamke kuwa ni binadamu kamili ungekuwa umempa haki sawa na zinazofanana na zile za mwanaume, maadamu haujafanya hivyo basi haumhesabu kuwa ni binadamu kamili.

USAWA AU KUFANANA?

Hoja hii imejengwa juu ya msingi kwamba kwa vile heshima ya binaadamu ni sawa kwa mwanaume na mwanamke, hivyo lazima wote wapate haki zinazofanana bila kujali majukumu yao katika maisha. Hapana shaka, utu na heshima yao ni sawa kwao wao wote; wote wanapaswa kuwa na haki sawa. Lakini vipi kuhusu kufanana kwa haki zao?

Ikiwa badala ya kufuata kibubusa mawazo ya Kimagharibi tutaamua kufikiri sisi wenyewe, swali la kwanza linalokuja akilini ni iwapo kweli haki sawa zinamaanisha haki zinazofanana.

Kwa kweli hayo ni mambo mawili tofauti. Usawa ni haki ya kuwa na daraja sawa kithamani na hadhi ambapo kufanana maana yake ni kulandana. Inawezekana baba akagawa mali zake kwa watoto wake watatu kwa usawa lakini sio kwa kulingana.

 

Jaalia mali yake inajumuisha vitu mbalimbali kama vile maduka, mashamba na baadhi ya mali zilizokodishwa. Baba kwa kuzingatia vipaji vyao na mambo ambayo kila mmoja anapenda, anaamua kumpa mmoja duka, mwingine shamba na wa tatu mali zilizokodishwa. Anazingatia kuwa thamani ya mali aliyopewa kila mmoja wao ni sawa na wengine na kila mmoja amepewa kutokana na kipaji chake. Hivyo aligawa mali yake kwa usawa lakini sio kwa kulingana.

Uwingi ni tofauti na ubora, na usawa ni tofauti na kufanana. Uislamu hauamini juu ya kulingana (uniformity) kwa mwanaume na mwanamke. Lakini wakati huo huo, hauwapendelei wanaume katika maswala ya haki. Umezingatia kanuni ya usawa kati ya mwanamke na mwanaume lakini haukubaliani na kufanana kwa haki zao.

Usawa ni neno linalifurahisha kwa sababu linaashiria hali ya kutobagua. Lina utukufu maalum. Linaamsha na kuleta heshima, hasa linapohusiana na haki.

Ni neno zuri lilioje ‘Usawa na Haki.’ Mtu yeyote mwema atafurahishwa na uzuri wake.

 

Lakini hatuwezi tukaelewa ni kwa jinsi gani mambo yalifika hatua hii kiasi cha kuwa wengine ambao walikuwa vinara wa sayansi na falsafa, nao wanataka kuingiza mawazo yao juu ya kufanana kwa haki kati ya wanawake na wanaume huku kwetu.

Hii ni sawa na mtu kuuza viazi vitamu kwa jina la mapeasi.

Hapana shaka kuwa Uislamu haujatoa haki zinazofanana kati ya mwanaume na mwanamke katika mambo yote. Lakini pia haujaamuru majukumu na adhabu zinazofanana kwa jinsia hizi mbili. Yote kwa yote ni kuwa, thamani ya jumla ya haki za mwanamke sio ndogo kuliko ile ya mwanaume. Tunataka kuthibitisha nukta hii.

Hapa linazuka swali, kwa nini haki za mwanaume na mwanamke hazijafanana katika mambo yote. Je isingekuwa vizuri zaidi kama haki zao zingekuwa zinafanana katika mambo yote? Ili kulijadili hili swali kikamilifu, tutajadili chini ya vichwa vya habari vitatu.

Mtazamo wa Uislamu juu ya nafasi ya mwanamke kutokana na maumbile yake.

Athari za tofauti za kimwili kati ya mwanaume na mwanamke. Je, hili linasababisha tofauti ya haki zao pia?

Ni nini falsafa ya sheria za Kiislamu, ambazo wakati fulani zinatofautisha kati ya mwanaume na mwanamke? Je, falsafa hii bado ni thabiti?

NAFASI YA MWANAMKE KATIKA UTARATIBU WA KIISLAMU.

Qur’ani sio mkusanyiko tu wa sheria. Sio chombo cha sheria na kanuni kavu bila maelezo ya madhumuni yake. Ina sheria na pia ina historia, mawaidha ya kidini, maelezo ya malengo ya maisha, na maelfu ya mambo mengine katika sehemu mbalimbali.

Qur’ani huelezea mambo yenye sura ya kisheria na katika sehemu nyingine hueleza lengo la maisha. Hufunua siri za dunia, mbingu, mimea, wanyama na wanadamu. Huelezea siri za maisha na kifo, heshima na aibu, kupanda na kushuka, mali na umaskini.

Qur’ani sio kitabu cha falsafa, lakini kimeelezea kwa ufasaha sana maoni yake (Qur’ani) juu ya falsafa ya masomo matatu ya msingi; Ulimwengu, mwanadamu na jamii. Haiwafundishi wafuasi wake sheria peke yake, na haijishughulishi na mawaidha na nasaha (maonyo) peke yake, bali kwa kupitia tafsiri yake ya maisha (maumbile), huwapa wafuasi wake mtazamo maalum na namna pekee ya kufikiri.

Msingi wa kanuni za Kiislamu juu ya masuala ya kijamii kama vile umiliki, serikali, haki za kifamilia n.k ni tafsiri ya maisha na mambo mengine tofauti tofauti.

Moja ya mambo yaliyoelezwa katika Qur’ani ni kuumbwa kwa mwanaume na mwanamke. Qur’ani haijakaa kimya juu ya jambo hili. Haijaacha mwanya kwa wadukuzi wa kifalsafa kuibua falsafa yao juu ya kanuni za mwanaume na mwanamke. Uislamu umetoa maoni yake juu ya mwanamke.

Ili kujua maoni ya Uislamu juu ya mwanamke, tutazame Qur’ani inachosema juu ya tabia yake ya ndani. Dini nyingine pia zimelizungumzia suala hili, lakini ni Qur’ani peke yake ambayo katika Aya kadhaa inaelezea waziwazi kuwa mwanamke ameumbwa kutokana na spishi za mwanaume, na wote mwanamke na mwanaume wana tabia za ndani zinazofanana.

Akimzungumzia Adam, Mwenyezi Mungu anasema;

“Yeye (Allah) aliwaumba nyinyi wote kutokana na nafsi moja, na kutokana nayo (hiyo nafsi moja) akamuumbia mwenza wake (Surat Nisaa 4:1).

Na juu ya mwanadamu kwa ujumla, Qur’ani inasema; “Amewaumbieni wake zenu kutokana na nyinyi.’ (Suratul Nisaa, Suratul Al Imran na Suratul Ruum).

Tofauti na vitabu vingine vya kidini hakuna sehemu yoyote katika Qur’ani ambapo imetajwa kuwa mwanamke ameumbwa kwa kutumia vitu duni au kuwa ana asili ya ukupe au ni wa asili ya upande wa kushoto. Uislamu hauungi mkono dhana ya kibiblia kuwa mwanamke ameumbwa kutokana na ubavu wa kushoto wa Adam. Uislamu hauna mtazamo wa dharau juu ya asili ya mwanamke na tabia zake za ndani.

Kuna nadharia nyingine ya dharau kwa wanawake iliyokuwa imeenea sana siku za nyuma, na imeacha alama mbaya katika siku za nyuma, na imeacha alama mbaya katika fasihi ya dunia. Kwa mujibu wa nadharia hiyo mwanamke anaonekana kuwa ndio chanzo cha madhambi yote. Kwamba kuwepo kwake tu, kunahamasisha uovu. Wengine wanadai kuwa mwanamke ni shetani mdogo.

Inasemekana kuwa katika kila dhambi na uhalifu uliotendwa na mwanaume kuna mkono wa mwanamke. Kwamba wanaume wenyewe hawatendi madhambi, ni wanawake wanaowasukumia kwenye madhambi.

Pia inasemekana kuwa shetani hawezi kumwendea mwanaume moja kwa moja. Ni kupitia mwanamke ndio huwapotosha wanaume. Shetani humchochea mwanamke na mwanamke humchochea mwanaume. Inaelezwa kuwa Adam aliondolewa peponi kwa sababu ya mwanamke. Kwamba Shetani alimshawishi Hawa, na ni Hawa aliyemshawishi Adam.

Qur’ani imesimulia kisa hiki cha peponi lakini hakuna iliposema kuwa shetani au nyoka alipompotosha Hawa na Hawa akampotosha Adam. Haimlaumu Hawa wala haimuondoi katika hatia.

Qur’ani inasema; “Tulimwambia Adam, ‘Kaa Peponi; wewe na mke wako, na kuleni humo matunda popote mpendapo lakini msiusogelee mti ule msije kuwa miongoni mwa madhalimu.” (Suratul Baqara, 2:35).

Inaweka kiwakilishi cha watu wawili. Pia Qur’ani inasema; “Kisha Shetani aliwatia wasiwasi.” “Naye akawaapia (kuwaambia) kwa hakika mimi ni mmoja wa watoao shauri njema kwenu. (Suratul Aaraf 7:20-21).

Hivyo Qur’ani inapinga vikali dhana ya uongo iliyokuwa imeenea sana wakati wa kuteremshwa Qur’ani na miwangwi, ambayo bado inasikika katika sehemu mbalimbali za dunia hii leo. Ilimuondoa mwanamke katika mashitaka kwamba yeye ni mchochezi wa dhambi na kwamba yeye ni shetani mdogo.

Nadharia nyingine ya dharau kwa mwanamke ambayo imekuwepo ni juu ya nafasi ya kiroho ya mwanamke. Ilidaiwa kuwa mwanamke hawezi kuingia peponi. Hana uwezo wa kiroho na msaada wa Mungu kumuwezesha kufanya hivyo. Hana uwezo wa kufikia ukaribu wa Mwenyezi Mungu kama mwanaume anavyoweza kufanya.

Lakini Qur’ani katika Aya mbalimbali imesema waziwazi kuwa malipo ya pepo na ukaribu na Mwenyezi Mungu havitegemei jinsia ya mtu. Inategemea na imani na amali (vitendo), na hakuna tofauti kati ya mwanamke na mwanaume juu ya hili katika Qur’ani, wametajwa watakatifu wa kiume na watakatifu wa kike.

Qur’ani imewatukuza wake wa Adam na Ibrahim na mama yake Nabii Isa na Musa.

Imewataja wake wa Nuhu na Lut kuwa hawakuwa stahili ya waume zao na haijamsahau mke wa Firauni, ambaye ametajwa kuwa ni mwanamke mtukufu aliyekuwa mikononi mwa mwanaume muovu. Katika visa vyake Qur’ani imeweka mizania. Mashujaa wake ni wa kiume na wa kike.

Wakati, ikimzungumzia mama yake Nabii Musa, Qur’ani inasema, “Tulimjulisha mama yake Musa kwa kumwambia: ‘Muweke katika sanduku na mtupe katika mto. Mawimbi yatamfikisha ufukweni. (Suratul Taha 20:39).

Juu ya mama yake Issa, Qur’ani inasema kuwa alifikia daraja tukufu ya kiroho kiasi kwamba malaika walikuwa wakiongea naye wakati anasali. Alikuwa akipokea chakula kutoka peponi. Daraja la kiroho lilimshangaza hata Zakaria, Mtume wa wakati huo.

Kumekuwa na mifano mingi ya wanawake mashuhuri na watakatifu katika historia ya Uislamu. Ni wanaume wachache tu wanaweza kufikia daraja la Khadija, mke kipenzi wa Mtume (s.a.w) na ni wachache mwanaume anayefikia daraja la bibi Fatima Zahra, binti kipenzi wa Mtume isipokuwa Mtume mwenyewe. Ana daraja kubwa kuliko hata la watoto wake ambao ni Maimamu.

Uislamu hauwabagui wanawake dhidi ya wanaume katika ‘safari ya kumuendea Allah’ isipokuwa humuona mwanaume kuwa mwenye kufaa zaidi kuchukua jukumu la utume, ambalo yaweza kuelezewa kama safari ya kurudi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwenda kwa watu.

Nadharia nyingine ya dharau kwa wanawake inahusiana na kujihini na kutooa/kutoolewa. Baadhi ya dini zinaona kuwa tendo la ndoa ni kitu kichafu, kwa mujibu wa imani ya wafuasi wake, wanaoweza kufikia kilele cha juu cha daraja la kiroho ni wale tu ambao watamaliza maisha yao yote bila kuoa/kuolewa.

Kiongozi mmoja wa dunia wa kidini anasema, “Kateni mti wa ndoa kwa shoka ya ubikira.’ Viongozi hawa wa kidini wanavumilia ndoa tu kama uovu wenye nafuu. Kwa maneno mengine wanashikilia kuwa, kwa kuwa watu wengi hawawezi maisha ya bila kuoa/kuolewa na inaeleweka kwamba hawataweza kujidhibiti na hivyo kujiingiza katika zinaa za wanawake/wanaume wengi, basi ni bora waoe ili wasije kukutana na mwanamke zaidi ya mmoja.

Watu hawa wanatetea kukaa bila kuoa au kuolewa na kujihini kwa sababu wanaona tendo la ndoa si kitu kizuri. Wanaona upendo kwa mwanamke kuwa ni uovu mkubwa wa kimaadili.

Uislamu unapinga vikali upuuzi huu. Unaiona ndoa kuwa ni taasisi tukufu na kukaa bila kuoa/kuolewa kuwa ni uchafu. Kumpenda mwanamke ni sehemu ya tabia ya Mtume. Mtukutu Mtume amesema; “Napenda vitu vitatu, manukato, mwanamke na swala.”

Bertrand Russel anasema, “Dini zote, isipokuwa Uislamu, zinalitazama tendo la ndoa kwa jicho baya. Uislamu unalitazama kwa maslahi ya kijamii, umeliwekea utaratibu maalum na kulidhibiti, lakini haulitazami kama uchafu.”

Nadharia nyingine ya dharau kwa mwanamke ni kuwa mwanamke ameumbwa kwa maslahi ya mwanaume.

Uislamu hausemi hivyo. Umeeleza malengo ya maisha kwa uwazi kabisa. Imeeleza kuwa dunia, mbingu, hewa, mawingu, mimea na wanyama vyote vimeumbwa kwa ajili ya mwanadamu. Haijasema mwanamke ameumbwa kwa ajili ya mwanaume. Kwa mujibu wa Qur’ani mwanaume ameumbwa kwa ajili ya mwanamke na mwanamke ameumbwa kwa ajili ya mwanaume.

 ‘Wao (wanawake) ni nguo zenu na nyinyi (wanaume) ni nguo zao (2:187).

Ingekuwa Qur’ani imeeleza kuwa mwanamke ni nyongeza (kiambatanisho) ya mwanaume na aliumbwa kwa ajili ya starehe yake (mwanaume), mtazamo huu ungekuwa umetazamwa katika sheria za Kiislamu, lakini Qur’ani haijasema hivyo. Hauyaelezei malengo ya maisha hivi. Haumuoni mwanamke kuwa ni kiambatanisho tu cha mwanaume. Ndio maana mtazamo huu haujazingatiwa katika sheria za Kiislamu.

Nadharia nyingine ya dharau kwa mwanamke ni kuwa mwanamke ni uovu usioepukika. Katika siku za nyuma, watu walimtazama mwanamke kwa dharau sana na walimuona kuwa ni chanzo cha mikosi na aina zote za matatizo.

Kinyume chake Qur’ani imesisitiza kuwa mwanamke ni baraka kwa mwanaume na ni chanzo cha raha na faraja kwake.Kwa mujibu wa nadharia nyingine ya dharau kwa mwanamke ni kuwa, hawakuthamini mchango wa mwanamke katika uzazi. Waarabu wa kabla ya Uislamu na baadhi ya jamii nyingine, waliomuona mwanamke kama mfuko tu wa kukuzia mbegu ya mwanaume. Sehemu mbalimbali za Qur’ani zimesema ‘Tumewaumba kutokanana na mwanaume na mwanamke.’ Wazo hili limeelezwa katika Aya nyingine za Qur’ani. Hivyo Uislamu ulikomesha fikra hiyo kuwa mwanamke ni mfuko tu wa kukuzia mbegu ya mwanaume.

Ni dhahiri sasa kuwa Uislamu hauna kabisa mitazamo yoyote ya kumdharau mwanamke.