Na Rajab Kusenge.

 

Siku chache baada ya kuondokewa na Mhadhiri nguli, Alhaji Saidi Omar Ricco, Taasisi ya Kimataifa ya Almalid, imepata pigo lingine.

Pigo hilo linatokana na kuondokewa na Mwenyekiti wao wa Tawi la Morogoro Sheikh Hussein Ally Msungi (72).

Mwenyekiti huyo aliyeitumikia Taasisi hiyo tangu miaka ya tisini, alifikwa na umauti Desemba 14 nyumbani kwake Mwembesongo na kuzikwa Desemba 15 mwaka huu  katika makaburi ya  Mafisa kwa Dala.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi, mtoto wa Marehemu Bwana Hassan Hussein Msungi, amesema kuwa kwa muda mrefu baba yake alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya kansa ya koo.

“Mzee alikuwa akisumbuliwa na kansa ya koo tangu mwaka jana na kupata matibabu hospitali mbalimbali mpaka umauti ulipomfika”, amesema mtoto huyo wa marehemu mara baada ya mazishi.

Msiba huo uliowakutanisha mamia ya Waislamu na wasiokuwa Waislamu ulihudhuriwa pia na Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Bakwata Sheikh Twaha Kilango.

Aidha Taasisi ya Almalid Taifa katika msiba huo iliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wahadhiri nchini pamoja na wahadhiri wengine kutoka ndani na nje ya mkoa wa Morogoro.

Baadhi ya Wahadhiri Mkoani humo wamemuelezea Sheikh Msungi alikuwa ni zaidi ya Mwenyekiti kwao katika suala zima la malezi na usimamizi wa shughuli za Daa’wa.

“Kwa upande wangu nasema pamoja na cheo chake cha uenyekiti, pia alikuwa mlezi kwetu sisi Wahadhiri wa Morogoro, naomba niseme maneno hayo machache tu lakini yamebeba maana nzima namna alivyokuwa Marhuum”, amesema kwa masikitiko Mhadhiri Athman Mataula.

Naye Mhadhir Hamis Rajab Dibagula amemuelezea Marehemu Sheikh Msungi kuwa alikuwa ni mlezi kwao wa kuigwa na walezi wengine kutokana na namna alivyoishi na Wahadhir wa rika zote.

“Kwetu ni pigo alikuwa Mwalimu, Kiongozi na mlezi aliyekuwa karibu na Wahadhiri wote na kwa hekima na busara zake tumeweza kuvuka vikwazo vingi katika harakati zetu hususani kwenye mihadhara ya dini linganishi”, amesema Dibagula ambaye alikuwa mhadhiri wa kwanza nchini kuhukumiwa kufungwa jela miezi 18 kwa kusema Yesu si Mungu.

Chini ya Marehemu Sheikh Msungi, Taasisi ya Almalid tawi la Morogoro imeweza kufanya kazi ya daa’wa ndani ya Manispaa hiyo na nje, ambapo maelfu ya watu wameweza kuijua dini ya Mwenyezi Mungu na wengi wao kuifuata.

Kwa kushirikiana na Umoja wa vijana wa Kiislamu Mkoani humo (JUSHUMUDI) chini ya mlezi wake Sheikh Ayub Salum Muinge, taasisi hiyo iliweza kupata nguvu ya kuanzisha tawi  kutokana na kufanya mihadhara mikubwa iliyowahusisha Wahadhiri maarufu kutoka Jijini Dares Salaam.

Kitovu kikubwa cha mihadhara hiyo mkoani humo kilikuwa msikiti wa kiwanja cha ndege (Mungu Mmoja Dini Moja) kabla ya kuhamia katika misikiti mingine ukiwemo wa Mwembesongo na viwanja vya wazi kikiwemo kile cha shule ya msingi Kikundi.

Mihadhara hiyo ikawa chachu ya Taasisi hiyo kufungua tawi Mkoani humo huku Wahadhiri wake wakijifunza kupitia kwa wenzao wa Dar es Salaam namna ya kulingania ndani na nje ya Misikiti kwa kutumia vitabu vitukufu vya Mwenyezi Mungu.

Aidha tukio la Msikiti wa uwanja wa ndege (Mungu Mmoja Dini Moja) kupigwa mabomu mwaka 1994 wakati Kikuni cha Almalid Taifa kikifanya mhadhara Msikitini hapo, nacho kikakachochea na kuleta shauku ya Waislamu wa Dar kuwa kaibu na wenzao wa Morogoro.

Lakini tukio lingine kubwa la kihistoria ambalo nalo lilichangia kwa kiasi kikubwa Taasisi hiyo kuamua kuwa na Tawi Mkoani Morogoro lilitokana na kadhia ya mabucha ya nguruwe ambapo Wahadhiri kadhaa walishikiliwa na polisi kisha kuhukumiwa kwenda jela miaka minne.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo Waislamu wa Morogoro chini ya mwavuli wa umoja wa Vijana JUSHUMUDI waliamua kwenda kusikiliza hukumu ya Wahadhiri hao kwa kutembea kwa miguu kutoka Morogoro mpaka Dar es Salaam.

Katika safari yao hiyo walifika usiku wa kuamkia hukumu ambapo walifikia Msikiti wa Mwembechai na kupokewa na Mamia ya Waislamu wakati wa swala ya Insha huku Marehemu Alahaji Said Ricco akiwa ameshika kipaza sauti na kuwatangazia Waislamu kuwa mashujaa kutoka Morogoro waliotembea kwa miguu wameshawasili, ambapo msikiti ulirindima kwa kivumo cha Takbira.

 

Sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.