Na Bakari Mwakangwale

IMEELEZWA kuwa katika uhai wake Sheikh Mustapha Khalid Swidiq, akiwa nchi za Kiarabu alikataa zawadi ya fedha na gari, badala yake alitaka msaada wa kujengewa Shule.

Kwa msimamo huo, Alhaji Sheikh Mustafa, aliyefariki Jumatano ya Machi 6, 2019, ametajwa kuwa ni mfano wa kuigwa kwa kutanguliza maslahi ya umma wa Kiislamu mbele badala ya maslahi yake binafsi, pamoja na kujua thamani ya elimu na kuifanyia kazi kwa vitendo.

Katika tukio hilo Sheikh Mustafa, aliambatana na baadhi ya Masheikh kutoka Tanzania kwa kuitikia wito katika nchi za Kiarabu kwa lengo la kwenda kuwekana sawa juu ya mgogoro mkubwa ulioibuka kwa Waislamu wa Kanda ya Ziwa.

Mgogoro huo maarufu ‘Mgogoro wa Ijumaa na Adhuhuri’ ulizua tafrani katika ukanda huo na kupelekea Serikali kuingilia kati na kufunga Misikiti zaidi ya 60 ya Ijumaa na Adhuhuri, ambayo Sheikh Mustafa alikua  Mufti wake.

Kwa mujibu wa msimuliaji wa kisa hicho, alisema mgogoro huo ulifika kwa Masheikh nchini Oman na baada ya kupatiwa fat’wa, timu ya Masheikh iliyotoka Tanzania kwenda kutafuta muafaka, akiwemo Sheikh Mustapha, walitakiwa kuchagua zawadi ili wawanunuliwe na kurudi nazo Tanzania, ambapo wengi walichagua vitu vizuri vya thamani vinavyopendwa na watu zaidi duniani.

“Sheikh Mustafa alistajabisha wageni na wenyeji kwa kutokua na haraka ya kusema yeye anataka zawadi gani, ulikua ni mshangao mkubwa pale Sheikh Mustafa, aliposema anachagua kujengewa Shule.”

Kwani walijua kujenga Shule ni mchakato mrefu na kufanya ionekane Sheikh (Mustafa) anarudi mikono mitupu, wengi walimsihi achukue gari au pesa, lakini Sheikh alishikilia msimamo wake wa kutaka kujengewa Shule.” Ameeleza msimuliaji.

Wakati Sheikh Mustafa, akitoa ombi hilo tayari alikuwa ana eneo (ardhi) takribani hekari 100, iliyopo Mujuga, umbali wa kilomita mbili kutoka ilipo Madrasa yake (Madrasat Falah).

Ambapo ombi la Sheikh Mustafa, lilitekelezwa kwa kukabidhiwa watu wa Islamic Development Bank (IDB), kujenga shule ya Sekondari, na mwaka 2003, Sekondari ya Kiislamu ya Katoro (Katoro Islamic) ilianza rasmi, huku Sheikh Mustapha akitoa sapoti kubwa katika mchakato mzima wa maendeleo ya Sekondari hiyo.

Kupitia, Sekondari hiyo ikiwa ni matunda ya ombi la Sheikh Mustafa, ndio imezaa vituo vingine vya elimu kama Chuo Cha Ualimu Katoro (Katoro Training Collage) na Shule ya Msingi Katoro (Katoro English Medium Primary Schoool) ambapo umma wa Kiislamu unanufaika kupata elimu kupitia vituo hivyo.

Kuhusu mgogoro wa ‘Ijumaa na Adhuhuri’ Sheikh Mustafa, alikuwa anaamini katika kuswali swala ya Ijumaa na Adhuhuri kwa wakati mmoja na kulikuwa na Misikiti zaidi ya Hamsini katika ukanda huo wa Mkoa wa Kagera inayofuata “fat’wa” yake hiyo.

Wakati fulani Serikali ilitaka kusuluhisha kwa kumtuma Makamo wa Rais Sheikh Aboud Jumbe, lakini Aboud Jumbe akarejea na taarifa kwamba mgogoro ule haukuwa wa kisiasa hivyo asingeuweza. Hapo akatumwa Sheikh Abdallah Saleh Farsy, aliyekuwahi kua Chief Kadhi wa Zanzibar na Kenya. Sheikh Farsy, alimaliza mgogoro kwa kutoa ‘rai’ kuwa wote wako sahihi na kila watu waendele na utaratibu wao.