Utafiti mpya unaonyesha kuwa, mgonjwa mmoja kati ya watano wa maradhi ya Covid-19

 

 

 

Utafiti mpya unaonyesha kuwa, mgonjwa mmoja kati ya watano wa maradhi ya Covid-19 anakumbwa na magonjwa ya kisaikolojia, ndani ya miezi mitatu baada ya kugundulika kuwa ameambukizwa ugonjwa huo.

Utafiti huo uliofanywa na Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza umebainisha kuwa, asilimia 20 ya watu waliopona Covid-19, huendelea kusumbuliwa na matatizo ya kiakili ndani ya siku 90.

Profesa Paul Harrison wa Chuo Kikuu cha Oxford amesema kuwa Sonona, msongo wa mawazo na ukosefu wa usingizi ni baadhi ya matatizo ya kiakili yanayowakumba wagonjwa wa corona waliopata afueni.

Amesema kuna haja kwa wanasayansi na madaktari kote duniani wachunguze kiini na matibabu ya matatizo ya kisaikolojia baada ya ugonjwa wa Covid-19.

Mwezi uliopita, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitadharisha juu ya ongezeko la watu wanaokumbwa na matatizo ya kisaikolojia barani Afrika, kutokana na athari hasi za janga la corona.

Kwa mujibu wa WHO, Kutengwa (karantini), kupoteza ajira, kuwapoteza wapendwa, pamoja na wimbi la taarifa za kweli na zisizo za kweli zinazohusu virusi vipya (vya corona) kunaweza kuongeza kiwango cha msongo wa mawazo na kusababisha matatizo ya kisaikolojia, au hata kuwazidishia mashaka wenye matatizo hayo.Parstoday.

 

Most Read

  • Week

  • Month

  • All